Matendo 26:19-32
Matendo 26:19-32 BHN
“Hivyo, mfalme Agripa, sikuweza kuwa mkaidi kwa maono hayo ya mbinguni. Ila nilianza kuhubiri kwanza kwa watu wa Damasko, halafu kwa wale wa Yerusalemu na nchi yote ya Yudea, na pia kwa watu wa mataifa mengine. Niliwahimiza wamgeukie Mungu na kuonesha kwa vitendo kwamba wamebadilisha mioyo yao. Kwa sababu hiyo, Wayahudi walinikamata nikiwa hekaluni, wakajaribu kuniua. Lakini Mungu alinisaidia; na hivyo mpaka siku ya leo nimesimama imara nikitoa ushuhuda kwa wote, wakubwa na wadogo. Ninayosema ni yale ambayo manabii na Mose walisema yatatukia; yaani ilimpasa Kristo ateseke na kuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu, ili atangaze kwamba mwanga wa ukombozi unawaangazia sasa watu wote, Wayahudi na pia watu wa mataifa mengine.” Paulo alipofika hapa katika kujitetea kwake, Festo alisema kwa sauti kubwa, “Paulo! Una wazimu! Kusoma kwako kwingi kunakutia wazimu!” Lakini Paulo akasema, “Sina wazimu mheshimiwa Festo. Ninachosema ni ukweli mtupu. Wewe Mfalme unayafahamu mambo haya, kwa hiyo ninaweza kuongea bila woga mbele yako. Sina mashaka kwamba matukio hayo yanajulikana kwako maana jambo hili halikutendeka mafichoni. Mfalme Agripa, je, una imani na manabii? Najua kwamba unaamini.” Agripa akamjibu Paulo, “Kidogo tu utanifanya Mkristo!” Paulo akamjibu, “Namwomba Mungu kwamba, kwa muda mfupi au mrefu, si wewe tu bali wote wanaonisikia leo wapate kuwa kama nilivyo mimi, lakini bila hii minyororo.” Hapo mfalme Agripa, mkuu wa mkoa, Bernike na wale wote waliokuwa pamoja nao, walisimama. Walipokwisha ondoka, waliambiana, “Mtu huyu hakufanya chochote kinachostahili adhabu ya kifo au kifungo.” Naye Agripa akamwambia Festo, “Mtu huyu angeweza kufunguliwa kama asingalikuwa amekata rufani kwa Kaisari.”