Matendo 26:19-32
Matendo 26:19-32 Biblia Habari Njema (BHN)
“Hivyo, mfalme Agripa, sikuweza kuwa mkaidi kwa maono hayo ya mbinguni. Ila nilianza kuhubiri kwanza kwa watu wa Damasko, halafu kwa wale wa Yerusalemu na nchi yote ya Yudea, na pia kwa watu wa mataifa mengine. Niliwahimiza wamgeukie Mungu na kuonesha kwa vitendo kwamba wamebadilisha mioyo yao. Kwa sababu hiyo, Wayahudi walinikamata nikiwa hekaluni, wakajaribu kuniua. Lakini Mungu alinisaidia; na hivyo mpaka siku ya leo nimesimama imara nikitoa ushuhuda kwa wote, wakubwa na wadogo. Ninayosema ni yale ambayo manabii na Mose walisema yatatukia; yaani ilimpasa Kristo ateseke na kuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu, ili atangaze kwamba mwanga wa ukombozi unawaangazia sasa watu wote, Wayahudi na pia watu wa mataifa mengine.” Paulo alipofika hapa katika kujitetea kwake, Festo alisema kwa sauti kubwa, “Paulo! Una wazimu! Kusoma kwako kwingi kunakutia wazimu!” Lakini Paulo akasema, “Sina wazimu mheshimiwa Festo. Ninachosema ni ukweli mtupu. Wewe Mfalme unayafahamu mambo haya, kwa hiyo ninaweza kuongea bila woga mbele yako. Sina mashaka kwamba matukio hayo yanajulikana kwako maana jambo hili halikutendeka mafichoni. Mfalme Agripa, je, una imani na manabii? Najua kwamba unaamini.” Agripa akamjibu Paulo, “Kidogo tu utanifanya Mkristo!” Paulo akamjibu, “Namwomba Mungu kwamba, kwa muda mfupi au mrefu, si wewe tu bali wote wanaonisikia leo wapate kuwa kama nilivyo mimi, lakini bila hii minyororo.” Hapo mfalme Agripa, mkuu wa mkoa, Bernike na wale wote waliokuwa pamoja nao, walisimama. Walipokwisha ondoka, waliambiana, “Mtu huyu hakufanya chochote kinachostahili adhabu ya kifo au kifungo.” Naye Agripa akamwambia Festo, “Mtu huyu angeweza kufunguliwa kama asingalikuwa amekata rufani kwa Kaisari.”
Matendo 26:19-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa hiyo, Ee Mfalme Agripa, sikuyaasi yale maono ya mbinguni, bali kwanza niliwahubiria wale wa Dameski na Yerusalemu, na katika nchi yote ya Yudea, na watu wa Mataifa, kwamba watubu na kumwelekea Mungu, wakiyatenda matendo yanayopatana na kutubu kwao. Kwa sababu ya hayo Wayahudi wakanikamata nikiwa ndani ya hekalu wakajaribu kuniua. Basi kwa kuwa nimeupata msaada utokao kwa Mungu nimesimama hata leo hivi nikiwashuhudia wadogo kwa wakubwa, wala sisemi neno ila yale ambayo manabii na Musa waliyasema, kwamba yatakuwa; ya kwamba Kristo hana budi kuteswa na ya kwamba yeye kwanza kwa kufufuliwa katika wafu atatangaza habari za nuru kwa watu wake na kwa watu wa Mataifa. Alipokuwa akijitetea hivi, Festo akasema kwa sauti kuu, Paulo, una wazimu, kusoma kwako kwingi kumekugeuza akili. Lakini Paulo akasema, Sina wazimu, Ee Festo mtukufu, bali nanena maneno ya kweli na ya akili kamili. Kwa maana mfalme anajua habari za mambo haya, nami naweza kusema naye kwa ujasiri, kwa sababu najua sana ya kuwa hapana neno moja katika hayo asilolijua; kwa maana jambo hilo halikutendeka pembeni. Mfalme Agripa, je! Wawaamini manabii? Najua ya kuwa wawaamini. Agripa akamwambia Paulo, Kwa maneno machache wadhani kunifanya mimi kuwa Mkristo. Paulo akamjibu, Namwomba Mungu kwamba, ikiwa kwa machache au ikiwa kwa mengi, si wewe tu ila na hao wote wanaonisikia leo wawe kama mimi, isipokuwa kuwa katika minyororo hii. Mfalme na mtawala na Bernike na wale walioketi pamoja nao wakasimama; hata walipoondoka wakasemezana, wakisema, Mtu huyu hatendi neno linalostahili kifo wala kufungwa. Agripa akamwambia Festo, Mtu huyo angeweza kufunguliwa, kama asingalitaka rufani kwa Kaisari.
Matendo 26:19-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa hiyo, Ee Mfalme Agripa, sikuyaasi yale maono ya mbinguni, bali kwanza niliwahubiri wale wa Dameski na Yerusalemu, na katika nchi yote ya Uyahudi, na watu wa Mataifa, kwamba watubu na kumwelekea Mungu, wakiyatenda matendo yanayopatana na kutubu kwao. Kwa sababu ya hayo Wayahudi wakanikamata ndani ya hekalu wakajaribu kuniua. Basi kwa kuwa nimeupata msaada utokao kwa Mungu nimesimama hata leo hivi nikiwashuhudia wadogo kwa wakubwa, wala sisemi neno ila yale ambayo manabii na Musa waliyasema, kwamba yatakuwa; ya kwamba Kristo hana budi kuteswa na ya kwamba yeye kwanza kwa kufufuliwa katika wafu atatangaza habari za nuru kwa watu wake na kwa watu wa Mataifa. Alipokuwa akijitetea hivi, Festo akasema kwa sauti kuu, Paulo, una wazimu, kusoma kwako kwingi kumekugeuza akili. Lakini Paulo akasema, Sina wazimu, Ee Festo mtukufu, bali nanena maneno ya kweli na ya akili kamili. Kwa maana mfalme anajua habari za mambo haya, nami naweza kusema naye kwa ujasiri, kwa sababu najua sana ya kuwa hapana neno moja katika hayo asilolijua; kwa maana jambo hilo halikutendeka pembeni. Mfalme Agripa, je! Wawaamini manabii? Najua ya kuwa wawaamini. Agripa akamwambia Paulo, Kwa maneno machache wadhani kunifanya mimi kuwa Mkristo. Paulo akamjibu, Namwomba Mungu kwamba, ikiwa kwa machache au ikiwa kwa mengi, si wewe tu ila na hao wote wanaonisikia leo wawe kama mimi, isipokuwa vifungo hivi. Mfalme na liwali na Bernike na wale walioketi pamoja nao wakasimama; hata walipoondoka wakasemezana, wakisema, Mtu huyu hatendi neno linalostahili kifo wala kufungwa. Agripa akamwambia Festo, Mtu huyo angeweza kufunguliwa, kama asingalitaka rufani kwa Kaisari.
Matendo 26:19-32 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Hivyo basi, Mfalme Agripa, sikuacha kuyatii yale maono yaliyotoka mbinguni, bali niliyatangaza kwanza kwa wale wa Dameski, kisha Yerusalemu na katika vijiji vyote vya Yudea na pia kwa watu wa Mataifa, kwamba inawapasa kutubu na kumgeukia Mungu na kuthibitisha toba yao kwa matendo yao. Ni kwa sababu hii Wayahudi walinikamata nilipokuwa Hekaluni, wakataka kuniua. Hadi leo nimepata msaada kutoka kwa Mungu, na hivyo nasimama hapa nikishuhudia kwa wakubwa na wadogo. Sisemi chochote zaidi ya yale ambayo manabii na Musa walisema yatatukia: kwamba Al-Masihi atateswa, na kwamba yeye atakuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu, na atatangaza nuru kwa watu wake na kwa watu wa Mataifa.” Paulo alipokuwa akifanya utetezi huu, Festo akasema kwa sauti kubwa, “Paulo, wewe umerukwa na akili! Kusoma kwingi kunakufanya uwe kichaa!” Lakini Paulo akajibu, “Mimi sijarukwa na akili, mtukufu sana Festo, bali nanena kweli nikiwa na akili zangu timamu. Naam, mfalme anajua kuhusu mambo haya yote, nami nasema naye kwa uhuru. Kwa sababu nina hakika kwamba hakuna hata mojawapo ya mambo haya asilolijua, kwa kuwa hayakufanyika mafichoni. Mfalme Agripa, je, unaamini manabii? Najua kuwa unaamini.” Agripa akamwambia Paulo, “Je, unanishawishi kwa haraka namna hii niwe mfuasi wa Al-Masihi?” Paulo akasema, “Ikiwa ni kwa haraka au la, namwomba Mungu, si wewe peke yako bali pia wale wote wanaonisikiliza leo, wawe kama mimi nilivyo, kasoro minyororo hii.” Baada ya kusema hayo, mfalme akainuka pamoja na mtawala na Bernike na wale waliokuwa wameketi pamoja nao. Walipokuwa wakiondoka, wakaambiana, “Mtu huyu hafanyi jambo lolote linalostahili kifo au kifungo.” Agripa akamwambia Festo, “Mtu huyu angeachwa huru kama hangekuwa amekata rufaa kwa Kaisari.”