Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 26

26
Paulo ajitetea mbele ya Agripa
1Ndipo Agripa akamwambia Paulo, “Una ruhusa kujitetea.”
Hivyo Paulo akawaashiria kwa mkono wake, akaanza kujitetea, akasema: 2“Mfalme Agripa, najiona kuwa na heri kusimama mbele yako leo ninapojitetea kuhusu mashtaka yote ya Wayahudi, 3hasa kwa sababu unajua vyema desturi zote za Kiyahudi na ya kuwa wewe unajua kwa undani mila na masuala ya mabishano. Kwa hiyo, nakusihi unisikilize kwa uvumilivu.
4“Wayahudi wote wanajua jinsi nilivyoishi tangu nilipokuwa mtoto, kuanzia mwanzo wa maisha yangu katika nchi yangu na pia huko Yerusalemu. 5Wao wamenifahamu kwa muda mrefu, na wanaweza kushuhudia wakipenda kushuhudia, kwamba kutokana na misimamo mikali sana ya dhehebu letu kwenye dini yetu, niliishi nikiwa Farisayo#26:5 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli.. 6Nami sasa ni kwa sababu ya tumaini langu katika kile ambacho Mungu aliwaahidi baba zetu, ninashtakiwa leo. 7Hii ndiyo ahadi ambayo makabila yetu kumi na mawili yanatarajia kuiona ikitimizwa wanapomtumikia Mungu kwa bidii usiku na mchana. Ee mfalme, ninashtakiwa na Wayahudi kwa ajili ya tumaini hili. 8Kwa nini yeyote miongoni mwenu afikiri kwamba ni jambo lisilosadikika Mungu kufufua wafu?
9“Mimi pia nilikuwa nimeshawishika kwamba imenipasa kufanya yote yale yaliyowezekana kupinga Jina la Isa Al-Nasiri. 10Nami hayo ndiyo niliyoyafanya huko Yerusalemu. Kwa mamlaka ya viongozi wa makuhani, niliwafunga watakatifu wengi gerezani, na walipokuwa wakiuawa nilipiga kura yangu kuunga mkono. 11Mara nyingi nilienda kutoka sinagogi#26:11 Nyumba ya ibada na mafunzo. moja hadi lingine nikiamuru waadhibiwe, nami nilijaribu kuwalazimisha wakufuru. Katika shauku yangu dhidi yao, hata nilienda miji ya kigeni ili kuwatesa.
Paulo aeleza kuhusu kuokoka kwake
(Matendo 9:1-19; 22:6-16)
12“Siku moja nilipokuwa katika mojawapo ya safari hizi nikiwa ninaenda Dameski, nilikuwa na mamlaka na agizo kutoka kwa kiongozi wa makuhani. 13Ilikuwa yapata adhuhuri, ee mfalme, nilipokuwa njiani, niliona nuru kutoka mbinguni iliyong’aa kuliko jua, ikatuangaza pande zote, mimi na wale niliokuwa pamoja nao. 14Wote tulianguka chini, nami nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya Kiebrania, ‘Sauli, Sauli, mbona unanitesa? Ni vigumu kwako kuupiga teke mchokoo.’
15“Nikauliza, ‘Ni nani wewe, Bwana?’
“Naye Bwana akajibu, ‘Ni mimi Isa unayemtesa. 16Sasa inuka usimame kwa miguu yako. Nimekutokea ili nikuteue uwe mtumishi na shahidi wa mambo ambayo umeyaona, na yale nitakayokuonesha. 17Nitakuokoa kutoka kwa watu wako na watu wa Mataifa ambao ninakutuma kwao, 18uyafumbue macho yao ili wageuke kutoka gizani waingie nuruni, na kutoka kwa nguvu za Shetani wamgeukie Mungu, ili wapate msamaha wa dhambi na sehemu miongoni mwa wale waliotakaswa kwa kuniamini mimi.’
19“Hivyo basi, Mfalme Agripa, sikuacha kuyatii yale maono yaliyotoka mbinguni, 20bali niliyatangaza kwanza kwa wale wa Dameski, kisha Yerusalemu na katika vijiji vyote vya Yudea na pia kwa watu wa Mataifa, kwamba inawapasa kutubu na kumgeukia Mungu na kuthibitisha toba yao kwa matendo yao. 21Ni kwa sababu hii Wayahudi walinikamata nilipokuwa Hekaluni, wakataka kuniua. 22Hadi leo nimepata msaada kutoka kwa Mungu, na hivyo nasimama hapa nikishuhudia kwa wakubwa na wadogo. Sisemi chochote zaidi ya yale ambayo manabii na Musa walisema yatatukia: 23kwamba Al-Masihi#26:23 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta. atateswa, na kwamba yeye atakuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu, na atatangaza nuru kwa watu wake na kwa watu wa Mataifa.”
Paulo aeleza juu ya kuhubiri kwake
24Paulo alipokuwa akifanya utetezi huu, Festo akasema kwa sauti kubwa, “Paulo, wewe umerukwa na akili! Kusoma kwingi kunakufanya uwe kichaa!”
25Lakini Paulo akajibu, “Mimi sijarukwa na akili, mtukufu sana Festo, bali nanena kweli nikiwa na akili zangu timamu. 26Naam, mfalme anajua kuhusu mambo haya yote, nami nasema naye kwa uhuru. Kwa sababu nina hakika kwamba hakuna hata mojawapo ya mambo haya asilolijua, kwa kuwa hayakufanyika mafichoni. 27Mfalme Agripa, je, unaamini manabii? Najua kuwa unaamini.”
28Agripa akamwambia Paulo, “Je, unanishawishi kwa haraka namna hii niwe mfuasi wa Al-Masihi?”
29Paulo akasema, “Ikiwa ni kwa haraka au la, namwomba Mungu, si wewe peke yako bali pia wale wote wanaonisikiliza leo, wawe kama mimi nilivyo, kasoro minyororo hii.”
30Baada ya kusema hayo, mfalme akainuka pamoja na mtawala na Bernike na wale waliokuwa wameketi pamoja nao. 31Walipokuwa wakiondoka, wakaambiana, “Mtu huyu hafanyi jambo lolote linalostahili kifo au kifungo.”
32Agripa akamwambia Festo, “Mtu huyu angeachwa huru kama hangekuwa amekata rufaa kwa Kaisari.”

Iliyochaguliwa sasa

Matendo 26: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia