Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 27

27
Paulo asafiri kwenda Rumi
1Ilipoamuliwa kwamba tungesafiri kwa meli kwenda Italia, Paulo na wafungwa wengine wakakabidhiwa kwa kiongozi mmoja wa askari aliyeitwa Juliasi, aliyekuwa wa Kikosi cha Walinzi wa Kaisari. 2Tulipanda meli iliyotoka Adramitio, iliyokuwa inakaribia kusafiri kwenda kwenye bandari zilizopo pwani ya jimbo la Asia, tukaanza safari yetu tukiwa pamoja na Aristarko, Mmakedonia kutoka Thesalonike.
3Kesho yake tukatia nanga Sidoni, naye Juliasi akamfanyia wema Paulo, akamruhusu aende kwa rafiki zake ili wamtimizie mahitaji yake. 4Kutoka huko tukaingia baharini tena na tukapita upande wa chini wa kisiwa cha Kipro kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. 5Baada ya sisi kuvuka bahari iliyo upande wa Kilikia na Pamfilia, tukafika Mira huko Likia. 6Huko yule kiongozi wa askari akapata meli ya Iskanderia ikielekea Italia, akatupandisha humo. 7Tukasafiri polepole kwa siku nyingi na kwa shida, hatimaye tukafika karibu na Nido. Kwa kuwa upepo wa mbisho ulituzuia tusiweze kushika mwelekeo tuliokusudia, tukapita chini ya Krete mkabala na Salmone. 8Tukaambaa na pwani kwa shida, tukafika sehemu iitwayo Bandari Nzuri, karibu na mji wa Lasea.
9Muda mwingi ulikuwa umepotea, na kusafiri baharini kulikuwa hatari, kwa sababu wakati huu ulikuwa baada ya Siku ya Kufunga#27:9 yaani Siku ya Upatanisho ambayo iliadhimishwa kwa kufunga (Walawi 16:29; Walawi 23:26-32). Hivyo Paulo akawaonya akasema, 10“Mabwana, naona kuwa hii safari ni yenye maafa na ya kuleta hasara kubwa kwa meli na shehena, pia kwa maisha yetu.” 11Lakini badala ya yule kiongozi wa askari kusikiliza yale Paulo aliyosema, akafuata zaidi ushauri wa nahodha na mwenye meli. 12Kwa kuwa ile bandari ilikuwa haifai kukaa wakati wa majira ya baridi, wengi wakashauri kwamba tuendelee na safari wakitarajia kufika Foinike na kukaa huko kwa majira ya baridi. Hii ilikuwa bandari iliyo katika kisiwa cha Krete ikikabili upande wa kusini-magharibi na kaskazini-magharibi.
Dhoruba baharini
13Upepo mtulivu ulipoanza kuvuma toka kusini, wakadhani kuwa wangeweza kufikia lengo lao, hivyo wakang’oa nanga na kusafiri wakipita kandokando ya pwani ya kisiwa cha Krete. 14Lakini baada ya muda mfupi, ikavuma tufani kubwa iitwayo Eurakilo#27:14 yaani upepo wa kaskazini-mashariki kutoka kisiwa cha Krete. 15Meli ikapigwa na dhoruba na haikuweza kushindana na ule upepo, tukarudishwa baharini upepo ulikokuwa unaelekea. 16Hatimaye tukisafiri kupita chini ya kisiwa kidogo kiitwacho Kauda, ambapo kwa kuwa tulikuwa tumekingiwa upepo na hicho kisiwa, tuliweza kwa shida kuifunga mashua ya kuokolea watu. 17Watu walipokwisha kuivuta mashua hiyo na kuiingiza katika meli, waliifunga kwa kamba chini ya meli yenyewe ili kuzishikanisha pamoja. Wakiogopa kupelekwa kwenye mchanga karibu na pwani ya Sirti, wakashusha matanga wakaiacha meli isukumwe na huo upepo. 18Tulikuwa tunapigwa na dhoruba kwa nguvu, kiasi kwamba kesho yake walianza kutupa shehena toka kwenye meli. 19Siku ya tatu, wakatupa vyombo vya meli baharini kwa mikono yao wenyewe. 20Wakati jua wala nyota hazikuonekana kwa siku nyingi, na dhoruba iliendelea kuvuma, hatimaye tulikata tamaa ya kuokolewa.
21Baada ya watu kukaa siku nyingi bila kula chakula, Paulo akasimama mbele yao na kusema: “Enyi watu, kama mngekubali ushauri wangu wa kutosafiri kwa meli kutoka Krete, basi mngejiepusha na uharibifu na hasara hii. 22Sasa ninawasihi sana, jipeni moyo kwa kuwa hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza maisha yake, ila meli itaangamia. 23Jana usiku, malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake na ninayemwabudu alisimama karibu nami, 24akaniambia, ‘Paulo usiogope, kwa kuwa ni lazima usimame mbele ya Kaisari, naye Mungu amekupa kwa neema uhai wa wote wanaosafiri pamoja nawe.’ 25Hivyo jipeni moyo, enyi watu, kwa kuwa ninamwamini Mungu kwamba yatakuwa kama vile alivyoniambia. 26Lakini hata hivyo meli yetu itakwama kwenye kisiwa fulani.”
Meli yavunjika
27Usiku wa kumi na nne ulipofika, tulikuwa bado tunasukumwa na upepo katika Bahari ya Adria. Ilipokuwa yapata usiku wa manane, mabaharia wakahisi kwamba walikuwa wanakaribia nchi kavu. 28Kwa hiyo wakapima kina cha maji na kukuta kilikuwa pima ishirini#27:28 Pima 20 ni kama mita 37.; baada ya kuendelea mbele kidogo, wakapima tena wakapata kina cha pima kumi na tano#27:28 Pima 15 ni kama mita 27.. 29Wakiogopa kwamba meli yetu ingegonga kwenye miamba, wakashusha nanga nne za nyuma ya meli, wakawa wanaomba kupambazuke. 30Katika jaribio la kutoroka kutoka kwa meli, mabaharia wakashusha mashua ya kuokolea watu baharini, wakijifanya kwamba wanaenda kushusha nanga za omo#27:30 au gubeti. 31Ndipo Paulo akamwambia yule jemadari na askari, “Hawa watu wasipobaki katika meli, hamtaweza kuokoka.” 32Hivyo basi wale askari wakakata kamba zilizoshikilia ile mashua ya kuokolea watu kwenye meli, wakaiacha ianguke humo baharini.
33Kabla ya mapambazuko, Paulo akawasihi watu wote wale chakula akisema, “Leo ni siku ya kumi na nne mmekuwa katika wasiwasi mkiwa mmefunga na bila kula chochote. 34Kwa hiyo nawasihi mle chakula, kwa maana itawasaidia ili mweze kuishi. Kwa kuwa hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza unywele hata mmoja kutoka kichwani mwake.” 35Baada ya kusema maneno haya, Paulo akachukua mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote, akaumega akaanza kula. 36Ndipo wote wakatiwa moyo, wakaanza kula chakula. 37Ndani ya meli tulikuwa jumla ya watu mia mbili na sabini na sita (276). 38Baada ya watu wote kula chakula cha kutosha, wakapunguza uzito wa meli kwa kutupa ngano baharini.
39Kulipopambazuka, mabaharia hawakuitambua ile nchi, lakini waliona ghuba yenye ufuko wa mchanga, ambako waliamua kuipweleza meli kama ingewezekana. 40Kwa hiyo wakatupa nanga zote na kuziacha baharini, na wakati huo huo wakalegeza kamba zilizokuwa zikishikilia usukani wa meli. Kisha wakatweka tanga la mbele lishike upepo na kuisukuma meli kuelekea pwani. 41Lakini wakafika mahali bahari mbili zinakutana, wakaipweleza meli ufuoni; omo ikakwama sana, ikawa haiwezi kuondolewa; lakini sehemu ya shetri#27:41 au tezi ikavunjika vipande vipande kutokana na kupigwa kwa mawimbi yenye nguvu.
42Wale askari wakapanga kuwaua wale wafungwa ili kuzuia hata mmoja wao asiogelee na kutoroka. 43Lakini yule jemadari alitaka kuokoa maisha ya Paulo, basi akawazuia askari wasitekeleze mpango wao. Akaamuru wale wanaoweza kuogelea wajitupe baharini kwanza, waogelee hadi nchi kavu. 44Waliosalia wangefika nchi kavu kwa kutumia mbao au vipande vya meli iliyovunjika, hivyo wote wakafika nchi kavu salama.

Iliyochaguliwa sasa

Matendo 27: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia