Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 11:21-35

Danieli 11:21-35 BHN

“ ‘Mfalme atakayefuata atakuwa baradhuli ambaye hana idhini ya kushika ufalme, naye atakuja bila taarifa na kunyakua ufalme kwa hila. Majeshi pamoja na kuhani wa hekalu, atawafagilia mbali na kuwaua. Kwa kufanya mapatano, atayahadaa mataifa mengine, na ataendelea kupata nguvu ingawa atatawala taifa dogo. Bila taarifa atazivamia sehemu za mkoa zenye utajiri mwingi na kufanya mambo ambayo hayakufanywa hata na mmoja wa wazee wake waliomtangulia. Kisha, atawagawia wafuasi wake mateka, mali na vitu alivyoteka nyara vitani. Atafanya mipango ya kuzishambulia ngome, lakini kwa muda tu. “ ‘Kwa ujasiri mwingi, ataunda jeshi kubwa ili kuushambulia ufalme wa kusini, naye mfalme wa kusini atajibu mashambulizi hayo kwa jeshi kubwa zaidi na lenye nguvu sana. Lakini, mfalme wa kusini hatafaulu kwani mipango ya hila itafanywa dhidi yake. Wale wanaokula pamoja naye, ndio watakaomwangamiza. Watamwangamiza na jeshi lake litafagiliwa mbali na wengi watauawa. Hapo wafalme hao wawili wataketi pamoja mezani kula, lakini kila mmoja anamwazia mwenzake uovu, na kudanganyana. Ila hawatafanikiwa, maana wakati uliopangwa utakuwa bado haujatimia. Mfalme wa kaskazini atarudi nchini mwake akiwa na mali nyingi, lakini nia yake moyoni ni kulitangua agano takatifu. Atafanya apendavyo, kisha atarudi katika nchi yake. “ ‘Katika wakati uliopangwa ataivamia nchi ya kusini kwa mara nyingine, lakini safari hii, mambo yatakuwa tofauti. Meli kutoka Kitimu zitamshambulia, naye atashikwa na hofu. Kisha atarudi nyuma huku amejaa hasira na atalitangua agano takatifu. Hapo atafuata shauri la wale walioasi agano takatifu. Wanajeshi wake watalitia najisi hekalu na ngome zake, watakomesha tambiko za kuteketezwa kila siku na kusimamisha huko hekaluni chukizo haribifu. Atawashawishi kwa hila wale walioasi agano, lakini watu walio waaminifu kwa Mungu wao watasimama imara na kuchukua hatua. Wenye hekima miongoni mwa watu watawafundisha wengi. Hata hivyo, kwa siku kadhaa watauawa kwa upanga au moto, watachukuliwa mateka au kunyanganywa mali zao. Wakati wanapouawa, watapata msaada kidogo, na wengi wanaojiunga nao, watafanya hivyo kwa unafiki. Baadhi ya wenye hekima watauawa, ili wapate kuondolewa uchafu, kutakaswa na kusafishwa, mpaka wakati wa mwisho, ambao sasa bado haujatimia.

Soma Danieli 11