Danieli 11:21-35
Danieli 11:21-35 NENO
“Atakayetawala baada yake atakuwa mtu wa kudharauliwa ambaye hajapewa heshima ya kifalme. Atauvamia ufalme wakati watu wake wanapojiona kuwa salama, naye atautwaa kwa hila. Ndipo jeshi kubwa litafagiliwa mbele yake; jeshi pamoja na mkuu mmoja wa agano wataangamizwa. Baada ya kufanya mapatano naye, atatenda kwa udanganyifu, na ataingia madarakani akitumia watu wachache tu. Wakati majimbo yaliyo tajiri sana yanajiona salama, atayavamia, naye atatimiza kile baba zake na babu zake hawakuweza. Atagawa nyara, mateka na utajiri miongoni mwa wafuasi wake. Atapanga njama ya kupindua miji yenye ngome, lakini kwa muda mfupi tu. “Atachochea nguvu zake na ushujaa wake kwa jeshi kubwa dhidi ya mfalme wa Kusini. Mfalme wa Kusini atafanya vita na jeshi kubwa lenye nguvu sana, lakini hataweza kusimama kwa sababu ya hila zilizopangwa dhidi yake. Wale wanaokula kutoka meza ya mfalme watajaribu kumwangamiza; jeshi lake litafagiliwa mbali, nao wengi watakufa vitani. Wafalme hawa wawili, mioyo yao ikiwa imekusudia mabaya, wataketi kwenye meza moja na kudanganyana wao kwa wao, lakini pasipo faida, kwa sababu bado mwisho utakuja katika wakati ulioamriwa. Mfalme wa Kaskazini atarudi katika nchi yake na utajiri mwingi, lakini atakuwa ameukaza moyo wake kinyume cha agano takatifu. Atachukua hatua dhidi ya hilo agano, kisha arudi nchi yake. “Wakati ulioamriwa, atavamia tena Kusini, lakini wakati huu matokeo yake yatakuwa tofauti na yale ya wakati wa kwanza. Meli za nchi ya Kitimu zitampinga, naye atavunjika moyo. Ndipo atarudi nyuma na kutoa hasira yake dhidi ya agano takatifu. Atarudi na kuonesha fadhili kwa wale wanaoliacha agano takatifu. “Majeshi yake yenye silaha yatainuka ili kunajisi ngome ya Hekalu, na kuondolea mbali sadaka ya kuteketezwa ya kila siku. Ndipo watalisimamisha chukizo la uharibifu linalosababisha ukiwa. Kwa udanganyifu, atapotosha wale walionajisi agano, lakini watu wanaomjua Mungu wao watampinga kwa uthabiti. “Wenye hekima watawafundisha wengi, ingawa kwa kitambo watauawa kwa upanga au kuchomwa moto, au kukamatwa, au kutekwa nyara. Watakapoanguka, watapokea msaada kidogo, nao wengi wasio waaminifu wataungana nao. Baadhi ya wenye hekima watajikwaa, ili waweze kusafishwa, kutakaswa na kufanywa wasio na waa hadi wakati wa mwisho, kwa maana bado litakuja kwa wakati ulioamriwa.