Danieli 11
11
1Nami katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Dario Mmedi, nilisimama kumsaidia na kumlinda.)
Wafalme wa kusini na kaskazini
2“Sasa basi, ninakuambia kweli: Wafalme wengine watatu watatokea Uajemi. Kisha atatokea mfalme wa nne, ambaye atakuwa tajiri sana kuliko wengine wote. Atakapokuwa amekwisha kujipatia nguvu kwa utajiri wake, atamchochea kila mmoja dhidi ya ufalme wa Uyunani. 3Ndipo mfalme mwenye nguvu atatokea, atakayetawala kwa nguvu nyingi, na kufanya anavyopenda. 4Baada ya kujitokeza, himaya yake itavunjwa na kugawanyika katika pande nne za mbinguni. Hautaenda kwa wazao wake, wala hautakuwa na nguvu alizokuwa nazo, kwa sababu himaya yake itang’olewa na kupewa wengine.
5“Mfalme wa Kusini atakuwa na nguvu, lakini mmoja wa majemadari wake atakuwa na nguvu zaidi yake, naye atatawala ufalme wake mwenyewe kwa nguvu nyingi. 6Baada ya miaka kadhaa, wataungana. Binti ya mfalme wa Kusini ataolewa kwa mfalme wa Kaskazini ili kuimarisha mapatano, lakini nguvu za huyo binti hazitadumu; hata mfalme hatadumu wala nguvu zake. Katika siku hizo atafukuzwa, pamoja na hao wasindikizaji wake wa kifalme, na baba yake, na yeyote aliyemuunga mkono.
7“Mmoja kutoka jamaa ya huyo binti atainuka na kuchukua nafasi yake. Atashambulia majeshi ya mfalme wa Kaskazini na kuingia katika ngome yake; atapigana dhidi yao, naye atashinda. 8Tena ataitwaa miungu yao, vinyago vyao vya chuma, na vitu vyao vya thamani vya fedha na dhahabu, na kuvichukua hadi Misri. Kwa miaka kadhaa atamwacha mfalme wa Kaskazini bila kumsumbua. 9Kisha mfalme wa Kaskazini atashambulia nchi ya mfalme wa Kusini, lakini atarudi hadi kwenye nchi yake mwenyewe. 10Wana wa mfalme wa Kaskazini watajiandaa kwa vita na kukusanya jeshi kubwa, ambalo litafagia nchi kama mafuriko yasiyozuilika, na kuendelea na vita hadi kwenye ngome ya mfalme wa Kusini.
11“Kisha mfalme wa Kusini atatoka kwa ghadhabu na kupigana dhidi ya mfalme wa Kaskazini, ambaye atakusanya jeshi kubwa, lakini litashindwa. 12Jeshi litakapotekwa, mfalme wa Kusini atajawa na kiburi, na atachinja maelfu mengi; hata hivyo hatabaki na ushindi. 13Kwa maana mfalme wa Kaskazini atakusanya jeshi kubwa kuliko lile la kwanza; baada ya miaka kadhaa, atasonga mbele na jeshi kubwa mno lililoandaliwa vizuri.
14“Katika nyakati hizo, wengi watainuka dhidi ya mfalme wa Kusini. Watu wenye ghasia miongoni mwa watu wako mwenyewe wataasi ili kutimiza maono, lakini bila mafanikio. 15Ndipo mfalme wa Kaskazini atakuja na kuuzingira mji kwa majeshi, na kuuteka mji wa ngome. Majeshi ya Kusini yatakosa nguvu za kumzuia; naam, hata vikosi vyao vya askari vilivyo bora zaidi, havitakuwa na nguvu za kuwakabili. 16Huyo mvamia nchi atafanya apendavyo; hakuna yeyote atakayeweza kumpinga. Atajiimarisha katika Nchi ya Kupendeza, na atakuwa na uwezo wa kuiangamiza. 17Ataamua kuja na nguvu za ufalme wake wote, na kufanya mapatano ya amani na mfalme wa Kusini. Naye atamtoa binti yake aolewe naye ili kuuangusha ufalme, lakini mipango yake haitafanikiwa wala kumsaidia. 18Ndipo atabadili nia yake na kupigana na nchi za pwani na aziteke nyingi, lakini jemadari mmoja atakomesha ufidhuli wake, na kurudisha ufidhuli wake juu yake. 19Baada ya hili atazigeukia ngome za nchi yake mwenyewe, lakini atajikwaa na kuanguka, wala hataonekana tena.
20“Atakayetawala baada yake atamtuma mtoza ushuru ili kudumisha fahari ya kifalme. Hata hivyo, baada ya miaka michache ataangamizwa, lakini si katika hasira wala katika vita.
21“Atakayetawala baada yake atakuwa mtu wa kudharauliwa ambaye hajapewa heshima ya kifalme. Atauvamia ufalme wakati watu wake wanapojiona kuwa salama, naye atautwaa kwa hila. 22Ndipo jeshi kubwa litafagiliwa mbele yake; jeshi pamoja na mkuu mmoja wa agano wataangamizwa. 23Baada ya kufanya mapatano naye, atatenda kwa udanganyifu, na ataingia madarakani akitumia watu wachache tu. 24Wakati majimbo yaliyo tajiri sana yanajiona salama, atayavamia, naye atatimiza kile baba zake na babu zake hawakuweza. Atagawa nyara, mateka na utajiri miongoni mwa wafuasi wake. Atapanga njama ya kupindua miji yenye ngome, lakini kwa muda mfupi tu.
25“Atachochea nguvu zake na ushujaa wake kwa jeshi kubwa dhidi ya mfalme wa Kusini. Mfalme wa Kusini atafanya vita na jeshi kubwa lenye nguvu sana, lakini hataweza kusimama kwa sababu ya hila zilizopangwa dhidi yake. 26Wale wanaokula kutoka meza ya mfalme watajaribu kumwangamiza; jeshi lake litafagiliwa mbali, nao wengi watakufa vitani. 27Wafalme hawa wawili, mioyo yao ikiwa imekusudia mabaya, wataketi kwenye meza moja na kudanganyana wao kwa wao, lakini pasipo faida, kwa sababu bado mwisho utakuja katika wakati ulioamriwa. 28Mfalme wa Kaskazini atarudi katika nchi yake na utajiri mwingi, lakini atakuwa ameukaza moyo wake kinyume cha agano takatifu. Atachukua hatua dhidi ya hilo agano, kisha arudi nchi yake.
29“Wakati ulioamriwa, atavamia tena Kusini, lakini wakati huu matokeo yake yatakuwa tofauti na yale ya wakati wa kwanza. 30Meli za nchi ya Kitimu zitampinga, naye atavunjika moyo. Ndipo atarudi nyuma na kutoa hasira yake dhidi ya agano takatifu. Atarudi na kuonesha fadhili kwa wale wanaoliacha agano takatifu.
31“Majeshi yake yenye silaha yatainuka ili kunajisi ngome ya Hekalu, na kuondolea mbali sadaka ya kuteketezwa ya kila siku. Ndipo watalisimamisha chukizo la uharibifu linalosababisha ukiwa. 32Kwa udanganyifu, atapotosha wale walionajisi agano, lakini watu wanaomjua Mungu wao watampinga kwa uthabiti.
33“Wenye hekima watawafundisha wengi, ingawa kwa kitambo watauawa kwa upanga au kuchomwa moto, au kukamatwa, au kutekwa nyara. 34Watakapoanguka, watapokea msaada kidogo, nao wengi wasio waaminifu wataungana nao. 35Baadhi ya wenye hekima watajikwaa, ili waweze kusafishwa, kutakaswa na kufanywa wasio na waa hadi wakati wa mwisho, kwa maana bado litakuja kwa wakati ulioamriwa.
Mfalme ajikwezaye mwenyewe
36“Mfalme atafanya apendavyo. Atajikweza na kujitukuza juu ya kila mungu, naye atasema mambo ambayo hayajawahi kusikiwa dhidi ya Mungu wa miungu. Atafanikiwa hadi wakati wa ghadhabu utimie, kwa maana kile kilichokusudiwa lazima kitatukia. 37Hataonesha heshima kwa miungu ya baba zake au kwa yule aliyetamaniwa na wanawake, wala hatajali mungu yeyote, bali atajikweza mwenyewe juu yao wote. 38Badala ya kuwajali miungu, ataheshimu mungu wa ngome; mungu ambaye hakujulikana na baba zake ndiye atamheshimu kwa dhahabu na fedha, kwa vito vya thamani, na zawadi za thamani kubwa. 39Atashambulia ngome zenye nguvu mno kwa msaada wa mungu wa kigeni, naye atawaheshimu sana wale watakaomkubali yeye. Atawafanya watawala wa watu wengi, na atagawa nchi kwa gharama.
40“Wakati wa mwisho, mfalme wa Kusini atapigana naye vita, naye mfalme wa Kaskazini atamshambulia kwa magari ya vita, askari wapanda farasi, na idadi kubwa ya meli. Atavamia nchi nyingi na kuzikumba nchi hizo kama mafuriko. 41Pia ataivamia Nchi ya Kupendeza. Nchi nyingi zitapinduliwa, bali Edomu, Moabu, na viongozi wa Amoni wataokolewa kutoka mkono wake. 42Atapanua mamlaka yake juu ya nchi nyingi; hata Misri haitaepuka. 43Atamiliki hazina za dhahabu na fedha na utajiri wote wa Misri, huku Walibia na Wakushi wakijisalimisha kwake. 44Lakini taarifa kutoka mashariki na kaskazini zitamshtua, naye ataondoka kwa ghadhabu nyingi ili kuangamiza na kuharibu wengi kabisa. 45Atasimika mahema yake ya ufalme kati ya bahari na mlima mtakatifu wa kupendeza. Hata hivyo, atafikia mwisho wake, wala hakuna yeyote atakayemsaidia.
Iliyochaguliwa sasa
Danieli 11: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.