Danieli 12
12
Nyakati za mwisho
1“Katika wakati huo Mikaeli, mtawala mkuu ambaye huwalinda watu wako, atainuka. Kutakuwako wakati wa taabu ambao haujatokea tangu mwanzo wa mataifa hadi wakati huo. Lakini wakati huo, watu wako, kila mmoja ambaye jina lake litakutwa limeandikwa kwenye kitabu, ataokolewa. 2Wengi ambao wamelala kwenye mavumbi wataamka, baadhi yao kwa uzima wa milele, wengine kwa aibu na kudharauliwa milele. 3Wale wenye hekima watang’aa kama mwanga wa mbingu, nao wale ambao huwaongoza wengi kutenda haki, watang’aa kama nyota milele na milele. 4Lakini wewe Danieli, yafunge na kuyatia muhuri maneno ya kitabu hiki hadi wakati wa mwisho. Wengi wataenda hapa na pale, na maarifa yataongezeka.”
5Ndipo mimi Danieli nikaangalia, nako mbele yangu walisimama wengine wawili, mmoja katika ukingo huu wa mto, na mwingine ukingo wa pili wa mto. 6Mmoja wao akamwambia yule mtu aliyevaa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, “Je, itachukua muda gani kabla mambo haya ya kushangaza hayajatimizwa?”
7Kisha mtu yule aliyevaa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, akainua mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto kuelekea mbinguni, nami nikamsikia akiapa kwa jina lake yeye aishiye milele, akisema, “Itakuwa wakati, nyakati mbili, na nusu wakati#12:7 Wakati, nyakati mbili na nusu wakati maana yake mwaka mmoja, miaka miwili, na nusu mwaka, yaani miaka mitatu na nusu.. Nguvu za watu watakatifu zitakapokuwa zimevunjwa kabisa, ndipo mambo haya yote yatakapotimizwa.”
8Nilisikia, lakini sikuelewa. Kwa hiyo nikauliza, “Bwana wangu, matokeo ya haya yote yatakuwa nini?”
9Akajibu, “Danieli, nenda zako, kwa sababu maneno haya yamefungwa na kutiwa muhuri hadi wakati wa mwisho. 10Wengi watatakaswa, na kuondolewa mawaa na kufanywa safi, lakini waovu wataendelea kuwa waovu. Hakuna mmoja wa waovu atakayefahamu, lakini wale wenye hekima watafahamu.
11“Tangu wakati ule wa kukomeshwa kwa dhabihu ya kila siku, na kuanzishwa kwa chukizo la uharibifu, kutakuwepo siku elfu moja na mia mbili na tisini (1,290). 12Kubarikiwa ni yule atakayevumilia hadi kufikia mwisho wa hizo siku elfu moja mia tatu na thelathini na tano (1,335).
13“Lakini wewe, nenda zako hadi mwisho. Utapumzika, nawe mwisho wa hizo siku utafufuka ili kuupokea urithi uliowekewa.”
Iliyochaguliwa sasa
Danieli 12: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.