Danieli 10
10
Maono ya Danieli kuhusu mtu
1Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Koreshi mfalme wa Uajemi, Danieli (ambaye aliitwa Belteshaza) alipewa ufunuo. Ujumbe wake ulikuwa kweli, nao ulihusu vita vikubwa. Ufahamu wa ujumbe ulimjia katika maono.
2Wakati huo, mimi Danieli nikaomboleza kwa majuma matatu. 3Sikula chakula kizuri; nyama wala divai havikugusa midomo yangu; nami sikujipaka mafuta kamwe hadi majuma matatu yalipotimia.
4Siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza, nilikuwa nimesimama kwenye ukingo wa mto mkubwa Hidekeli#10:4 yaani Mto Tigrisi. 5Nikatazama juu, na mbele yangu palikuwa na mtu aliyevaa mavazi ya kitani na mshipi wa dhahabu safi kutoka Ufazi kiunoni mwake. 6Mwili wake ulikuwa kama zabarajadi safi, uso wake kama radi, macho yake kama miali wa moto, mikono yake na miguu yake kama mng’ao wa shaba iliyosuguliwa, nayo sauti yake kama ya umati mkubwa wa watu.
7Ni mimi Danieli peke yangu niliyeona hayo maono; watu waliokuwa pamoja nami hawakuyaona, lakini waligubikwa na hofu kuu, hata wakakimbia na kujificha. 8Kwa hiyo niliachwa peke yangu, nikitazama maono hayo makubwa; sikubakiwa na nguvu, na rangi ya uso wangu ikabadilika kama aliyekufa, nikakosa nguvu. 9Kisha nikamsikia akisema, nami nilipokuwa nikimsikiliza, nikapatwa na usingizi mzito, nikalala kifudifudi.
10Mkono ulinigusa, ukaninyanyua na kuniweka magotini, mikono yangu ikishika chini, huku nikiwa bado ninatetemeka. 11Akasema, “Danieli, wewe mtu upendwaye sana, fikiri kwa makini maneno ninayoenda kunena nawe; simama wima, kwa maana sasa nimetumwa kwako.” Aliponiambia haya, nikasimama nikitetemeka.
12Ndipo akaendelea kusema, “Danieli, usiogope. Tangu siku ya kwanza ulipotia moyo wako kupata ufahamu na kujinyenyekeza mbele ya Mungu wako, maneno yako yalisikiwa, nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako. 13Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga kwa siku ishirini na moja. Ndipo Mikaeli, mmoja wa malaika wakuu, alikuja kunisaidia, kwa sababu nilikuwa nimezuiliwa huko na mfalme wa Uajemi. 14Sasa nimekuja kukuelezea mambo yatakayowatokea watu wako wakati ujao, kwa maana maono hayo yanahusu wakati ambao haujaja bado.”
15Alipokuwa akiniambia haya, nilisujudu, uso wangu ukigusa chini, nikawa bubu. 16Ndipo mmoja aliyeonekana kama mwanadamu akanigusa midomo yangu, nami nikafungua kinywa changu, nikaanza kunena. Nikamwambia yule aliyesimama mbele yangu, “Nimepatwa na huzuni kubwa kwa sababu ya maono haya, bwana wangu, nami nimeishiwa nguvu. 17Bwana wangu, mimi mtumishi wako nitawezaje kuzungumza na wewe? Nguvu zangu zimeniishia, hata ninashindwa kupumua.”
18Tena yule aliyeonekana kama mwanadamu akanigusa na kunitia nguvu. 19Akasema, “Ee mtu upendwaye sana, usiogope. Amani iwe kwako! Uwe na nguvu sasa; jipe nguvu.”
Alipozungumza nami, nilipata nguvu, nikasema, “Nena, bwana wangu, kwa kuwa umenipa nguvu.”
20Kwa hiyo akasema, “Je, unajua kwa nini nimekujia? Sasa hivi nitarudi kupigana dhidi ya mkuu wa Uajemi, nami nikienda, mkuu wa Uyunani atakuja. 21Lakini kwanza nitakuambia kile kilichoandikwa katika Kitabu cha Kweli. (Hakuna hata mmoja anayenisaidia dhidi yao isipokuwa Mikaeli, mkuu wenu.
Iliyochaguliwa sasa
Danieli 10: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.