Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 9

9
Maombi ya Danieli
1Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Dario mwana wa Ahasuero (mzaliwa wa Umedi), ambaye alifanywa mtawala wa ufalme wa Babeli, 2katika mwaka wa kwanza wa utawala wake, mimi Danieli nilielewa kutokana na Maandiko, kulingana na neno la Mwenyezi Mungu lililopewa nabii Yeremia, kwamba ukiwa wa Yerusalemu ungetimizwa kwa miaka sabini. 3Kwa hiyo nikamgeukia Mwenyezi Mungu na kumsihi katika maombi na dua, katika kufunga, na kuvaa gunia na kujipaka majivu.
4Nikamwomba Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, na kutubu:
“Ee Bwana, Mungu mkuu na unayetisha, anayeshika agano lake la upendo kwao wanaompenda na kutii maagizo yake, 5tumetenda dhambi na kufanya mabaya. Tumekuwa waovu na tumeasi; tumegeuka mbali na maagizo yako na sheria zako. 6Hatukuwasikiliza watumishi wako manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, wakuu wetu, baba zetu, na watu wote wa nchi.
7“Bwana, wewe ni mwenye haki, lakini siku hii ya leo tumefunikwa na aibu: watu wa Yuda, na wakaaji wa Yerusalemu, na Waisraeli wote, walio karibu na walio mbali, katika nchi zote ulikotutawanya kwa sababu tulikosa uaminifu kwako. 8Ee Mwenyezi Mungu, sisi na wafalme wetu, wakuu wetu na baba zetu tumefunikwa na aibu kwa sababu tumefanya dhambi dhidi yako. 9Bwana Mungu wetu ni mwenye rehema na anayesamehe, hata ingawa tumefanya uasi dhidi yake. 10Hatukumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, wala kuzishika sheria alizotupatia kupitia kwa watumishi wake, manabii. 11Israeli wote wamekosea sheria yako na kugeuka mbali, nao wamekataa kukutii.
“Kwa hiyo laana na viapo vya hukumu vilivyoandikwa katika Torati ya Musa, mtumishi wa Mungu, vimemiminwa juu yetu, kwa sababu tumefanya dhambi dhidi yako. 12Umetimiza maneno uliyosema dhidi yetu na dhidi ya watawala wetu, kwa kuleta maafa makubwa juu yetu. Chini ya mbingu yote kamwe hapajatendeka kitu kama kile kilichotendeka kwa Yerusalemu. 13Kama vile ilivyoandikwa katika Torati ya Musa, misiba hii yote imekuja juu yetu, lakini hatujaomba fadhili za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwa kuacha kutenda dhambi na kuisikiliza kweli yake. 14Mwenyezi Mungu hakusita kuleta maafa juu yetu, kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, ni mwenye haki katika kila afanyalo; lakini hata hivyo, hatujamtii.
15“Sasa, Ee Bwana Mungu wetu, uliyewatoa watu wako Misri kwa mkono wenye nguvu, na kujifanyia Jina linalodumu hadi leo, tumetenda dhambi, tumefanya mabaya. 16Ee Bwana, kwa kadiri ya matendo yako ya haki, ondoa hasira yako na ghadhabu yako kwa Yerusalemu, mji wako, mlima wako mtakatifu. Dhambi zetu na maovu ya baba zetu yameifanya Yerusalemu na watu wako kitu cha kudharauliwa kwa wale wote wanaotuzunguka.
17“Basi Mungu wetu, sasa sikia maombi na dua za mtumishi wako. Ee Bwana, kwa ajili yako angalia kwa huruma ukiwa wa mahali pako patakatifu. 18Ee Mungu, tega sikio, ukasikie; fumbua macho yako ukaone ukiwa wa mji ule wenye Jina lako. Hatukutolei maombi yetu kwa sababu sisi tuna haki, bali kwa sababu ya rehema zako nyingi. 19Ee Bwana, sikiliza! Ee Bwana, samehe! Ee Bwana, sikia na ukatende! Kwa ajili yako, Ee Mungu wangu, usikawie, kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa Jina lako.”
Majuma sabini
20Basi, nilipokuwa bado nikinena na kuomba, nikiungama dhambi yangu na dhambi ya watu wangu Israeli, na nikifanya maombi yangu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, kwa ajili ya mlima wake mtakatifu, 21wakati nilipokuwa bado katika maombi, Jibraili, yule mtu niliyekuwa nimemwona katika maono hapo awali, alinijia kwa kasi karibu wakati wa kutoa dhabihu ya jioni. 22Akanielimisha na kuniambia, “Danieli, sasa nimekuja kukupa akili na ufahamu. 23Mara ulipoanza kuomba, jibu lilitolewa, ambalo nimekuja kukupasha habari, kwa maana wewe unapendwa sana. Kwa hiyo, tafakari ujumbe huu na uelewe maono haya:
24“Majuma sabini yameamriwa kwa ajili ya watu wako na kwa ajili ya mji wako mtakatifu, ili kumaliza makosa, kukomesha dhambi, kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu, kuleta haki ya milele, kutia muhuri maono na unabii, na pia kumpaka mafuta yeye aliye mtakatifu sana.
25“Ujue na kuelewa hili: Tangu kutolewa kwa amri ya kuutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu hadi kuja kwa Mpakwa mafuta, aliye mtawala, kutakuwa na majuma saba, na majuma sitini na mawili. Barabara zitajengwa tena pamoja na mahandaki, lakini katika wakati wa taabu. 26Baada ya majuma sitini na mawili, Mpakwa Mafuta atakatiliwa mbali, wala hatabaki na kitu. Watu wa mtawala atakayekuja watauharibu mji pamoja na mahali patakatifu. Mwisho utakuja kama mafuriko: Vita vitaendelea hadi mwisho, nao ukiwa umeamriwa. 27Mtawala huyo atathibitisha agano na watu wengi kwa juma moja. Katikati ya juma hilo atakomesha dhabihu na sadaka. Mahali pa dhabihu katika Hekalu, atasimamisha chukizo la uharibifu, hadi mwisho ulioamriwa utakapomiminwa juu yake yeye aletaye uharibifu.”

Iliyochaguliwa sasa

Danieli 9: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia