Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 8

8
Maono ya Danieli ya kondoo dume na beberu
1Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Mfalme Belshaza, mimi Danieli nilipata maono, baada ya maono yaliyokuwa yamenitokea awali. 2Katika maono yangu, nilijiona nikiwa ndani ya ngome ya Shushani katika jimbo la Elamu; katika maono nilikuwa kando ya Mto Ulai#8:2 huu ni mfereji uliopitia kati ya Shushani. 3Nikatazama juu, na hapo mbele yangu kulikuwa na kondoo dume mwenye pembe mbili, akiwa amesimama kando ya mto, nazo pembe zake zilikuwa ndefu. Pembe moja ilikuwa ndefu kuliko hiyo nyingine, lakini iliendelea kukua baadaye. 4Nikamtazama yule kondoo dume alivyokuwa akishambulia kuelekea magharibi, kaskazini na kusini. Hakuna mnyama yeyote aliyeweza kusimama mbele yake, wala hakuna aliyeweza kuokoa kutoka nguvu zake. Akafanya kama alivyopenda, naye akawa mkuu.
5Nilipokuwa ninatafakari hili, ghafula beberu mwenye pembe moja kubwa katikati ya macho yake alikuja kutoka magharibi, akiruka kasi juu ya dunia yote bila kugusa ardhi. 6Alikuja akimwelekea yule kondoo dume mwenye pembe mbili niliyemwona akisimama kando ya mto, akamshambulia kwa hasira nyingi. 7Nikamwona akimshambulia yule kondoo dume kwa hasira nyingi, akampiga yule kondoo dume na kuvunja pembe zake mbili. Yule kondoo dume hakuwa na nguvu za kumzuia yule beberu; huyo beberu akamwangusha yule kondoo dume chini na kumkanyaga, wala hakuna aliyeweza kumwokoa yule kondoo dume kutoka nguvu za huyo beberu. 8Yule beberu akawa mkubwa sana, lakini katika kilele cha nguvu zake, ile pembe yake ndefu ilivunjika, na mahali pake pakaota pembe nne kubwa kuelekea pande nne za dunia.
9Kutoka mojawapo ya zile pembe nne palitokea pembe ndogo, nayo ikaongezeka nguvu kuelekea kusini, na mashariki, na Nchi ya Kupendeza. 10Pembe hiyo ikaendelea kukua hadi kufikia jeshi la mbinguni, nayo ikalitupa baadhi ya nyota za jeshi la angani chini duniani, na kuzikanyaga. 11Pembe hiyo ikajikweza ili iwe kama Mkuu wa hilo jeshi la Mwenyezi Mungu; ikamwondolea Mwenyezi Mungu dhabihu ya kila siku, napo mahali pake patakatifu pakashushwa chini. 12Kwa sababu ya uasi, jeshi la watakatifu na dhabihu za kila siku vikatiwa mkononi mwake. Pembe hiyo ikafanikiwa katika kila kitu ilichofanya, nayo kweli ikatupwa chini.
13Kisha nikamsikia mtakatifu mmoja akizungumza na mtakatifu mwingine, akamwambia, “Je, itachukua muda gani maono haya yatimie: maono kuhusu dhabihu ya kila siku, uasi unaosababisha ukiwa, kutwaliwa kwa mahali patakatifu, na jeshi litakalokanyagwa chini ya nyayo?”
14Akaniambia, “Itachukua jioni na asubuhi elfu mbili na mia tatu; ndipo mahali patakatifu patawekwa wakfu tena.”
Tafsiri ya maono hayo
15Mimi Danieli nilipokuwa ninaangalia maono na kujaribu kuelewa, mbele yangu alisimama mmoja aliyefanana na mwanadamu. 16Kisha nikasikia sauti ya mwanadamu kutoka Mto Ulai ikiita, “Jibraili, mwambie mtu huyu maana ya maono haya.”
17Alipokuwa akikaribia pale nilipokuwa nimesimama, niliogopa, nikaanguka kifudifudi. Akaniambia, “Mwana wa mwanadamu, fahamu kuwa maono haya yanahusu siku za mwisho.”
18Alipokuwa akinena nami, nilikuwa katika usingizi mzito, huku nimelala kifudifudi. Ndipo aliponigusa na kunisimamisha wima.
19Akaniambia, “Nitakuambia yale yatakayotokea baadaye wakati wa ghadhabu, kwa sababu maono haya yanahusu wakati wa mwisho ulioamriwa. 20Kondoo dume mwenye pembe mbili ambaye ulimwona anawakilisha wafalme wa Umedi na Uajemi. 21Yule beberu mwenye manyoya mengi ni mfalme wa Uyunani, nayo ile pembe ndefu katikati ya macho yake ni mfalme wa kwanza. 22Zile pembe nne zilizoota badala ya ile pembe iliyovunjika zinawakilisha falme nne ambazo zitatokea kutoka taifa lake, lakini hakuna hata mmoja utakaokuwa na nguvu kama ile pembe iliyovunjika.
23“Katika sehemu ya mwisho ya utawala wao, waasi watakapokuwa waovu kabisa, atainuka mfalme mwenye uso mkali, aliye stadi wa hila. 24Atakuwa na nguvu nyingi, lakini si kwa uwezo wake mwenyewe. Atasababisha uharibifu wa kutisha, na atafanikiwa kwa chochote anachofanya. Atawaangamiza watu maarufu na watu watakatifu. 25Atasababisha udanganyifu ustawi, naye atajihesabu mwenyewe kuwa bora kuliko wote. Wakati watajisikia kuwa salama, atawaangamiza wengi, na kushindana na Mkuu wa wakuu. Lakini ataangamizwa, isipokuwa si kwa uwezo wa mwanadamu.
26“Maono kuhusu jioni na asubuhi ambayo umepewa ni kweli, lakini yatie muhuri maono haya, kwa maana yanahusu nyakati za baadaye sana.”
27Mimi Danieli nilikuwa nimechoka sana, na nikalala nikiwa mgonjwa kwa siku kadhaa. Ndipo nikaamka, nikaendelea na shughuli za mfalme. Nilifadhaishwa na maono hayo; sikuweza kuyaelewa.

Iliyochaguliwa sasa

Danieli 8: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia