Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu la Sheria 28:45-57

Kumbukumbu la Sheria 28:45-57 BHN

“Hayo yote yatawapateni nyinyi na kuwaandama mpaka muangamizwe kwa kuwa hamkutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu kuhusu kushika amri zake na masharti aliyowapa. Lakini hizo zitakuwa ushahidi wa hukumu ya Mwenyezi-Mungu kwenu na wazawa wenu milele. “Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwabariki katika kila njia, lakini nyinyi hamkumtumikia kwa moyo wa furaha na mkunjufu. Kwa hiyo mtawatumikia maadui zenu ambao Mwenyezi-Mungu atawatuma dhidi yenu, kwa njaa, kiu na uchi, na kutindikiwa kila kitu. Atawafungeni nira ya chuma mpaka awaangamize. “Mwenyezi-Mungu ataleta kutoka mbali taifa moja liwavamie kasi kama tai, taifa ambalo lugha yake hamuielewi. Taifa hilo lenye watu wa nyuso katili halitajali wazee wala kuwahurumia vijana; litakula ng'ombe wenu na mazao yenu, mpaka mmeangamizwa. Halitawaachieni nafaka, divai, mafuta, ng'ombe au kondoo mpaka liwaangamize. Watu hao watawazingira katika miji yenu yote, mpaka kuta zenu za ngome ambazo mlitegemea zimeporomoshwa chini kila mahali katika nchi yenu ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewapeni. Wakati wa kuzingirwa na kutaabishwa na maadui wenu, mtakula watoto wenu ambao Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu amewapeni. Hata mtu mpole kabisa na aliyelelewa vizuri sana atamnyima chakula ndugu yake, mkewe ampendaye na mtoto wake atakayesalia; wala hatamgawia hata mmoja wao nyama ya watoto wake atakaowala. Hamtabakiwa na chochote wakati huo wa kuzingirwa na kutaabishwa na maadui katika miji yenu yote. Hata mwanamke yule ambaye ni mpole sana na aliyelelewa vizuri na mwororo hata hajawahi kukanyaga udongo kwa kisigino chake hataweza kufanya vingine. Wakati huo wa kuzingirwa kutakuwa na njaa hata atamla mtoto wake mchanga na kile kinachotoka baada ya kuzaliwa mtoto bila hata mumewe mpenzi au mmoja wa watoto wake kutambua.