Kumbukumbu 28:45-57
Kumbukumbu 28:45-57 NENO
Laana hizi zote zitakuja juu yako. Zitakufuatia na kukupata hadi uangamizwe, kwa sababu hukumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kuzishika amri zake na maagizo yake aliyokupa. Zitakuwa ishara na ajabu kwako na kwa wazao wako milele. Kwa sababu hukumtumikia Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa furaha na kwa moyo wakati wa kufanikiwa kwako, kwa hiyo katika njaa na kiu, katika uchi na umaskini wa kutisha, utawatumikia adui ambao Mwenyezi Mungu atawatuma dhidi yako. Yeye ataweka nira ya chuma shingoni mwako hadi amekwisha kukuangamiza. Mwenyezi Mungu ataleta taifa dhidi yako kutoka mbali, kutoka miisho ya dunia, kama tai ashukavyo chini, taifa ambalo hutaijua lugha yake, taifa lenye uso mkali lisilojali wazee wala kuwahurumia vijana. Watakula wadogo wa mifugo yako na mazao ya nchi yako hadi umeangamia. Hawatakuachia nafaka, divai mpya au mafuta, wala ndama wowote wa kundi lako au wana-kondoo wa kundi lako hadi umekuwa magofu. Nao wataizingira miji yote katika nchi yako, hata kuta ndefu za ngome ambazo unazitegemea zimeanguka. Watazingira miji yote katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wako, anakupa. Utakula uzao wa tumbo lako, nyama ya wana wako wa kiume na wa kike, ambao Mwenyezi Mungu, Mungu wako, amekupa, kwa sababu ya mateso yale adui zako watakayokuletea wakati wa kukuzingira. Hata yule mtu muungwana sana na makini miongoni mwako hatakuwa na huruma kwa ndugu yake mwenyewe au kwa mke ampendaye au watoto wake waliosalia, naye hatampa hata mmoja wao nyama ya watoto wake ambao anawala. Kwa kuwa hakuna kitu kingine kilichosalia kwake katika mazingirwa makali ambayo adui yako watakuletea kwa miji yako yote. Mwanamke ambaye ni muungwana sana na makini miongoni mwako, yaani ambaye ni makini sana na muungwana kiasi kwamba asingethubutu kugusa ardhi kwa wayo wa mguu wake, yeye atakuwa mchoyo kwa mume ampendaye na mwanawe mwenyewe au binti yake, kondoo wa nyuma kutoka tumbo lake na watoto anaowazaa. Kwa kuwa anakusudia kuwala kwa siri wakati wa kuzingirwa na katika taabu zile adui yako atazileta juu yako na miji yako.