Kumbukumbu la Sheria 32:1-14
Kumbukumbu la Sheria 32:1-14 BHN
“Tegeni masikio enyi mbingu: Sikiliza, ee dunia, maneno ninayosema. Mafundisho yangu na yatone kama mvua, maneno yangu yadondoke kama umande, kama manyunyu kwenye mimea michanga, kama mvua nyepesi katika majani mabichi. Maana nitalitangaza jina la Mwenyezi-Mungu, nanyi mseme, ‘Mungu wetu ni Mkuu’. “Mwenyezi-Mungu ni Mwamba wa usalama; kazi zake ni kamilifu, njia zake zote ni za haki. Yeye ni Mungu mwaminifu asiye na kosa, yeye hufanya mambo ya uadilifu na ya haki. Lakini nyinyi mmekosa uaminifu kwake, nyinyi sio watoto wake tena kwa sababu ya uovu, nyinyi ni kizazi kiovu na kipotovu. Mnawezaje kumlipa hivyo Mwenyezi-Mungu, enyi watu wapumbavu na msio na akili? Je, yeye siye Baba yenu aliyewaumba, aliyewafanya na kuwaimarisha? Kumbukeni siku zilizopita, fikirieni miaka ya vizazi vingi; waulizeni baba zenu nao watawajulisha, waulizeni wakubwa wenu nao watawaeleza. Mungu Mkuu alipoyagawia mataifa mali yao, alipowagawa wanadamu, kila taifa alilipatia mipaka yake, kulingana na idadi ya watoto wa Mungu, lakini alijiwekea watu wa Yakobo kuwa wake, hao alijichagulia kuwa mali yake. Aliwakuta katika nchi ya jangwa, nyika tupu zenye upepo mkali. Aliwalinda na kuwatunza, aliwafanya kama mboni ya jicho lake. Kama tai alindaye kiota chake, na kurukaruka juu ya makinda yake, akitandaza mabawa yake ili kuwashikilia, na kuwabeba juu ya mabawa yake. Yeye Mwenyezi-Mungu mwenyewe aliwaongoza na hapakuwa na mungu mwingine wa kumsaidia. Aliwapitisha katika nyanda za juu za nchi, nao wakala mazao ya mashambani. Akawapa asali miambani waonje na mafuta kutoka mwamba mgumu. Aliwapa siagi na maziwa ya mifugo, mafuta ya wanakondoo na kondoo madume, makundi ya mifugo ya Bashani na mbuzi. Aliwapa ngano nzuri kabisa na divai mpya wakanywa.