Kutoka 12:21-28
Kutoka 12:21-28 BHN
Basi, Mose akawaita wazee wote wa Waisraeli, akawaambia, “Chagueni kila mmoja wenu, kulingana na jamaa yake, mwanakondoo na kumchinja kwa sikukuu ya Pasaka. Mtachukua majani ya husopo na kuyachovya katika damu ndani ya birika na kupaka kwenye vizingiti na miimo yote miwili ya milango ya nyumba zenu. Mtu yeyote asitoke nje ya nyumba usiku huo hadi asubuhi. Maana mimi Mwenyezi-Mungu nitapita kuwaua Wamisri. Lakini nitakapoiona damu iliyopakwa kwenye vizingiti na miimo ya nyumba zenu, nitazipita na wala sitamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zenu na kuwaua. Shikeni jambo hilo nyinyi na wazawa wenu kama agizo la milele. Mtakapoingia katika nchi ile ambayo mimi Mwenyezi-Mungu nitawapa, kama nilivyoahidi, ni lazima kulitekeleza. Kila wakati watoto wenu watakapowauliza, ‘Jambo hili lina maana gani?’ Nyinyi mtawajibu, ‘Hii ni tambiko ya Pasaka kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu, kwa sababu alizipita nyumba za Waisraeli nchini Misri alipowaua Wamisri, lakini sisi hakutuua.’” Waisraeli wakainamisha vichwa na kumwabudu Mwenyezi-Mungu. Kisha Waisraeli wakaenda, wakafanya kama walivyoambiwa na Mose na Aroni kulingana na amri ya Mwenyezi-Mungu.