Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 16:15-34

Ezekieli 16:15-34 BHN

“Lakini, ulitegemea uzuri wako, ukatumia sifa yako kwa kufanya uzinzi, ukifanya umalaya na mtu yeyote apitaye. Ulitwaa baadhi ya mavazi yako, ukayatumia kupambia mahali pako pa ibada na hapo ndipo ukafanyia uzinzi wako. Jambo la namna hiyo halijapata kutokea wala halitatokea kamwe! Vito vyako vizuri vya dhahabu na fedha nilivyokupa, ulivitwaa, ukajifanyia sanamu za wanaume upate kufanya uzinzi nazo. Ukatwaa mavazi niliyokupa yaliyotiwa nakshi na kuzifunika zile sanamu, na mafuta yangu na ubani wangu, ukazitolea sanamu hizo. Chakula changu nilichokupa, ulikitoa kwa sanamu hizo kuwa harufu ya kupendeza kwani nilikulisha kwa unga safi, mafuta na asali. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema! “Tena, watoto wako wa kiume na wa kike ulionizalia uliwatwaa, ukazitambikia sanamu zako kwa kuwateketeza. Je, unadhani uzinzi wako ulikuwa ni jambo dogo? Je, jambo hili la kuwachinja watoto wangu ili wawe tambiko ya kuteketeza kwa ajili ya sanamu zako ni jambo dogo? Katika machukizo yako yote pamoja na uzinzi wako hukuzikumbuka siku za utoto wako, wakati ulipokuwa uchi kabisa, bila kitu, ukigaagaa katika damu yako! “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nakuambia: Ole wako, ole wako Yerusalemu! Baada ya kufanya hayo yote ulijijengea majukwaa ya ibada na mahali pa juu kila mahali. Mwanzoni mwa kila barabara ulijijengea mahali pa juu, ukautumia urembo wako kufanya uzinzi ukijitoa kwa kila mpita njia na kuongeza uzinzi wako. Tena ulifanya uzinzi na jirani zako Wamisri waliojaa tamaa, ukaongeza uzinzi wako na kuichochea hasira yangu. Basi, niliunyosha mkono wangu kukuadhibu. Nilipunguza chakula chako, nikakuacha kwa maadui zako, binti za Wafilisti ambao waliona aibu mno juu ya tabia yako chafu mno. “Kwa kuwa hukutosheka, ulifanya tena uzinzi na Waashuru. Na hiyo pia haikukutosheleza. Ulijitoa wewe mwenyewe utumiwe na Wababuloni, watu wafanyao biashara! Hata hivyo hukutosheka. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema, kweli wewe ni mgonjwa wa mapenzi. Unafanya uzinzi bila kuona haya hata kidogo. Umejijengea jukwaa lako mwanzoni mwa kila barabara na kujijengea mahali pa juu katika kila mtaa. Tena wewe hukuwa kama malaya kwani ulikataa kulipwa. Ulikuwa mke mzinzi akaribishaye wageni badala ya mumewe. Kwa kawaida wanaume huwalipa malaya, lakini wewe umewalipa wapenzi wako wote, ukiwahonga waje kwako toka pande zote upate kuzini nao. Katika umalaya wako hukufanya kama wanawake wengine: Hakuna aliyekubembeleza ili uzini naye bali wewe ulilipa fedha badala ya kulipwa.