Ezekieli 40:1-27
Ezekieli 40:1-27 BHN
Mwaka wa ishirini na tano tangu kuhamishwa kwetu, siku ya kumi ya mwezi wa kwanza, siku hiyo niliusikia uzito wa nguvu ya Mwenyezi-Mungu. Ilikuwa mwaka wa kumi na nne tangu mji wa Yerusalemu ulipotekwa. Basi, nikiwa katika njozi Mwenyezi-Mungu alinichukua mpaka nchini Israeli, akaniweka juu ya mlima mrefu sana, na upande wa kusini kulikuwa na majengo yaliyoonekana kama mji. Basi, alinipeleka huko, nami nikamwona mtu aliyeonekana anangara kama shaba. Mikononi mwake mtu huyo alikuwa na kamba ya kitani ya kupimia pamoja na ufito wa kupimia, naye alikuwa amesimama karibu na lango. Basi, akaniambia: “Wewe mtu! Tazama vizuri na kusikiliza kwa makini. Zingatia kwa moyo uone kila kitu nitakachokuonesha maana umeletwa hapa ili nikuoneshe kitu. Unapaswa kuwatangazia watu wa Israeli kila kitu utakachoona.” Basi, huko, niliona hekalu nalo lilikuwa limezungukwa na ukuta upande wa nje. Yule mtu akauchukua ufito wake wa kupimia ambao ulikuwa na urefu wa mita 3, akaupima ule ukuta. Ukuta huo ulikuwa na kimo cha mita 3 na unene wa mita 3. Kisha, akaenda kwenye lango la mashariki akapanda ngazi na akiwa juu akapima kizingiti cha lango ambacho kilikuwa na kina mita 3. Kulikuwa na vyumba vya walinzi kila upande wa nafasi ya kupitia na kila kimoja kilikuwa cha mraba: Urefu mita 3 upana mita 3. Kuta zilizotenganisha vyumba hivyo zilikuwa na unene mita 2.5. Kulikuwa na ukumbi mrefu wa mita 3 ambao ulielekea kwenye chumba kikubwa mkabala na hekalu. Yule mtu akakipima pia chumba hicho, nacho kilikuwa na kina mita 4. Halafu akapima kuta zake za nje zikaonekana zina unene wa mita moja. Sehemu ya ndani ya lango ilikuwa sehemu iliyokuwa karibu zaidi na hekalu. Kulikuwa na sehemu ya kuingilia iliyokuwa na vyumba vitatu vya walinzi, kila upande na vyote vilikuwa na ukubwa uleule; nazo kuta zilizovitenganisha zilikuwa na unene uleule. Kisha, yule mtu akapima upana wa nafasi ya kupitia katika lango. Upana wake ulikuwa mita 6.5. Ukubwa wote wa ukumbi wa katikati wa kupitia ulikuwa mita 5. Mbele ya vyumba vya walinzi ambavyo vilikuwa mraba: Mita 3 kwa 3, kulikuwa na ukuta mfupi kama kizuizi ukiwa na kimo cha sentimita 50 na unene sentimita 50. Yule mtu akapima umbali kutoka ukuta wa nyuma wa chumba kimojawapo hadi kwenye ukuta wa nyuma ya chumba upande wa pili penye nafasi ya kupitia, akapata mitakumi na mbili u nusu. Chumba cha mwisho kabisa kilielekea kwenye ua. Akakipima chumba hicho nacho kilikuwa na upana mita 10. Kutoka mbele ya lango kwenye mwingilio mpaka ukumbi wa ndani wa lango kulikuwa na mita 25. Kulikuwa na matundu madogomadogo kwenye miimo ya nje ya vyumba vyote na hata kwenye kuta zilizotenganisha vyumba. Kulikuwa na michoro ya mitende kwenye miimo ya ndani iliyoelekea ukumbi wa kupitia. Kisha yule mtu akanipeleka mpaka ua wa nje ya hekalu. Huko kulikuwa na vyumba thelathini kuuzunguka ukuta wa nje na mbele ya vyumba hivyo kulikuwa na sakafu ya mawe. Sakafu hiyo ilitandazwa kuzunguka malango kwa kufuatana na urefu wa malango hayo; hiyo ilikuwa sakafu ya chini. Baadaye, yule mtu akapima umbali wa njia iliyokuwa ikitoka kwenye ua wa ndani wa sehemu ya chini ikielekea nje ya ua huo, akapata mita 50. Kisha, yule mtu akapima urefu na upana wa lango la upande wa kaskazini wa ua wa nje. Kulikuwa na vyumba vitatu vya walinzi kila upande wa lango, vipimo vya miimo yake na matao yake vilikuwa kama vile vya lango la kwanza. Urefu wote wa ile njia ulikuwa kwa jumla mita 25 na upana wake mita kumi na mbili u nusu. Chumba cha kuingilia na madirisha na matao yake, pia ile mitende iliyochorwa ukutani, vyote vilifanana na vile vya lango la mashariki. Hapo palikuwa na ngazi saba za kupandia kwenye lango, na matao yake yalikuwa mbele yake. Kutoka hapo penye njia ya kuingilia ya kaskazini na kuvuka huo ua moja kwa moja kulikuwa na njia nyingine ya kuingilia iliyoelekea kwenye ua wa ndani, kama ilivyokuwa upande wa mashariki. Yule mtu alipima urefu wa kutoka njia mpaka njia, akapata mita 50. Yule mtu akanichukua upande wa kusini; huko nako kulikuwako lango; alipima miimo yake na ukumbi na vipimo vyake vilikuwa sawa na miimo na kumbi nyingine. Kulikuwa na madirisha pande zote kama ilivyokuwa katika vyumba vingine. Urefu wake ulikuwa mita 25 na upana wake mita kumi na mbili u nusu. Kulikuwa na ngazi saba za kupandia kwenye njia hiyo ya kuingilia na mwishoni mwake kulikuwa na ukumbi uliokuwa mkabala na ua. Kulikuwa na michoro ya mitende kwenye kuta za ndani zilizokuwa mkabala na hiyo njia ya kuingilia. Mkabala na njia hiyo ya kuingilia kulikuwa na njia ya kuingilia kwenye ua wa ndani. Yule mtu akapima urefu kati ya hizo njia, akapata mita 50.