Mwanzo 42:14-28
Mwanzo 42:14-28 BHN
Lakini Yosefu akawaambia, “Ni kama nilivyosema: Nyinyi ni wapelelezi tu. Hivi ndivyo mtakavyojaribiwa: Naapa kwa jina la Farao, kwamba hamtatoka hapa mpaka mdogo wenu atakapokuja. Mtumeni mmoja wenu akamlete huyo ndugu yenu mdogo, wakati wengine wenu wanamngoja gerezani. Hapo ndipo maneno yenu yatakapojulikana ukweli wake. La sivyo, naapa kwa jina la Farao kwamba nyinyi ni wapelelezi.” Kisha akawatia wote gerezani kwa muda wa siku tatu. Siku ya tatu Yosefu akawaambia, “Kwa kuwa mimi ni mcha Mungu, fanyeni hivi ili mpate kuishi: Kama kweli nyinyi ni watu waaminifu, mmoja wenu na abaki kifungoni, na wengine wawapelekee nafaka jamaa zenu wenye njaa. Kisha mleteni kwangu ndugu yenu mdogo. Hii itathibitisha ukweli wa maneno yenu, nanyi hamtauawa.” Basi, wakakubali kufanya hivyo. Kisha wakasemezana wao kwa wao, “Kweli sisi tulimkosea ndugu yetu. Ingawa tulimwona akisononeka rohoni mwake, sisi hatukumjali hata alipotusihi. Ndiyo maana taabu hii yote inatupata.” Reubeni akawaambia, “Je, mimi sikuwaambieni tusimdhuru kijana? Lakini nyinyi hamkunisikiliza! Sasa tunaadhibiwa kwa ajili ya damu yake.” Wao hawakujua kuwa Yosefu alielewa yote hayo waliyosema, maana alipoongea nao ilikuwa kwa njia ya mkalimani. Yosefu akaenda kando, akaangua kilio. Alipotulia, akarudi kuzungumza nao. Kisha akamkamata Simeoni na kumtia pingu mbele ya macho yao. Yosefu akatoa amri mifuko yao ijazwe nafaka, kila mmoja wao arudishiwe fedha yake katika gunia lake, na wapewe chakula cha njiani. Wakafanyiwa mambo hayo yote. Wakawatwisha punda wao mizigo yao ya nafaka, wakaondoka. Ikawa walipofika mahali pa kulala wageni huko njiani, mmoja wao akafungua gunia lake ili apate kumlisha punda wake, akashangaa kukuta fedha yake mdomoni mwa gunia lake. Akawaambia ndugu zake, “Fedha yangu imerudishwa. Hii hapa mdomoni mwa gunia langu!” Waliposikia hayo, wakafa moyo. Wakatazamana huku wanatetemeka na kuulizana, “Ni jambo gani hili alilotutendea Mungu?”