Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waebrania 4

4
1Basi, kwa vile ahadi ya kuingia mahali pa pumziko bado ipo, na tuogope ili yeyote kati yenu asije akashindwa kupata pumziko hilo. 2Maana Habari Njema imehubiriwa kwetu kama vile ilivyohubiriwa kwa hao watu wa kale. Lakini ujumbe huo haukuwafaa chochote, maana waliusikia lakini hawakuupokea kwa imani. 3#Taz Zab 95:11 Basi, sisi tunaoamini tunapata pumziko hilo aliloahidi Mungu. Kama alivyosema:
“Nilikasirika, nikaapa:
‘Hawataingia mahali pangu pa pumziko.’”
Mungu alisema hayo ingawa kazi yake ilikuwa imekwisha malizika tangu alipoumba ulimwengu. 4Maana Maandiko yasema mahali fulani kuhusu siku ya saba: “Mungu alipumzika siku ya saba, akaacha kazi zake zote.” 5#Taz Zab 95:11 Tena jambo hili lasemwa pia: “Hawataingia mahali pangu pa pumziko.” 6Basi, hiyo ahadi ya kuingia bado ipo, maana wale waliohubiriwa Habari Njema pale awali walishindwa kuingia humo kwa sababu walikosa kutii. 7#Taz Zab 95:7-8 Mungu aliweka siku nyingine ambayo inaitwa “Leo,” akasema baadaye kwa njia ya Daudi maneno yaliyokwisha tajwa:
“Kama mkisikia sauti ya Mungu leo,
msiwe wakaidi.”
8Kama Yoshua angekuwa amewapa watu hao hilo pumziko, Mungu hangalisema baadaye juu ya siku nyingine. 9Kwa hiyo, basi, bado kuna kupumzika kwa watu wa Mungu. 10Maana, kila aingiaye mahali pa pumziko la Mungu atapumzika kutoka katika kazi yake kama vile pia Mungu alivyopumzika kutoka kazi yake. 11Basi, tujitahidi kuingia katika pumziko hilo, ili asiwepo yeyote miongoni mwetu atakayekataa kutii kama walivyofanya wao.
12Neno la Mungu ni hai na lina nguvu; ni kali kuliko upanga wenye makali kuwili. Hukata kabisa mpaka mahali ambapo moyo na roho hukutana, mpaka pale vikutanapo viungo vya mwili na uboho. Neno hilo huchambua nia na fikira za mioyo ya watu. 13Hakuna kiumbe chochote kilichofichika mbele ya Mungu; kila kitu kimefunuliwa wazi mbele ya macho yake yeye ambaye kwake tutapaswa kutoa hoja ya matendo yetu.
Yesu Kuhani Mkuu
14Basi, tuzingatie kwa makini imani tunayoiungama. Maana tunaye Kuhani Mkuu aliyeingia mpaka mbinguni; Yesu, Mwana wa Mungu. 15Huyu Kuhani Mkuu wetu anaelewa kabisa unyonge wetu; yeye mwenyewe alijaribiwa kama sisi kwa kila namna lakini hakutenda dhambi. 16Basi, na tukikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu mwenye neema, tupokee huruma na neema ya kutusaidia wakati wa shida.

Iliyochaguliwa sasa

Waebrania 4: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia