Waebrania UTANGULIZI
UTANGULIZI
Mtu akiisoma “Barua” hii kwa uangalifu ataona waziwazi kwamba hii si barua bali ni simulizi la mahubiri. Kweli barua hii kwa Waebrania yaishia kama barua za nyakati hizo na maneno kadha wa kadha ya salamu, lakini tangu mwanzo hatuambiwi nani ameandikiwa “barua” hii wala nani aliiandika. Yawezekana kwamba “barua” hii ilipelekwa huko ilikopelekwa kutoka Italia (13:24). Wanaoandikiwa ni Wakristo wanaokabiliwa na matatizo hata kushawishiwa kuiacha imani yao ya Kikristo. Mwandishi anawatia moyo wabaki imara katika imani hiyo kwa kuwaonesha ukuu na upeo wa kazi ya Kristo kwa ajili ya wokovu. Tangu mwanzo wa maandishi haya tunahakikishiwa kwamba Mungu amejidhihirisha kwetu kikamilifu katika nafsi yake Yesu Kristo (1:1-3).
Simulizi la kitheolojia la maandishi haya kwa Waebrania linaendelezwa kwa kuchambua maana ya Agano la Kale kwa mwanga wa nafsi na kazi yake Yesu Kristo ambaye, kwa njia ya kafara yake yeye mwenyewe msalabani, ameleta wokovu kwa ulimwengu (Yoh 3:16-17). Kwake Kristo Yesu, Mungu alikamilisha ufunuo wake, ambao alikuwa ameudhihirisha kiasi fulani kwa mababu wa Waisraeli, kwa njia ya manabii (1:1). Barua hii kwa Waebrania inatilia mkazo hali ya pekee ya nafsi ya Yesu, Mwana wa Mungu, naye ni mkuu kuliko vitu vyote (1:2-4), kuliko malaika (1:4–2:18) kuliko Mose (3:1–4:13). Ukuhani wake wapita ule wa Walawi (4:14–7:28). Aghalabu Yesu ni Kuhani Mkuu ambaye aliingia mpaka mbinguni (4:14); yeye “ametufungulia njia mpya” (10:20). Tofauti na sheria ya Mose na tambiko zake za aina aina na ambazo ilibidi zifanyike mara nyingi, Yesu Kristo kwa mwili wake alijitoa kafara “mara moja tu kwa ajili ya kuziondoa dhambi za wengi” (9:26-28; 10:10,14).
Sehemu kubwa sana inatumiwa kueleza tambiko, ibada na wadhifa wa kikuhani katika Agano la Kale ili kuonesha upungufu wake na kuporomoka kwake, na hivyo kuonesha dhahiri zaidi umuhimu wa nafsi yake Yesu Kristo, ambaye kifo chake kimewaondelea watu dhambi zao. Katika muundo huo wa masimulizi yake, mwandishi anataja pia mambo ya kuzingatia katika maisha ya waumini: Maonyo dhidi ya kukosa imani na dhidi ya ukaidi kwa Mungu na kuanguka tena katika dhambi (2:1-4; 3:7-19; 4:11-13; 5:11–6:20; 10:26-39). Vile vile anawatia moyo wadumu katika imani na wasife moyo (10:19-25; 12:1-13).
Sura 10:19–13:17 Kwa jumla zinawahimiza wasomaji wadumu katika imani. Hapa tunayo ile sehemu maalumu inayowataja watu mashuhuri wa Agano la Kale kama mfano mzuri wa watu wenye imani. Baada ya hayo mwandishi anawataka wawe na matumaini thabiti kwa Yesu Kristo ili waweze kustahimili mapingamizi kama yeye. Kisha “barua” hiyo inamaliza kwa mawaidha na maonyo pamoja na kuwatakia wasomaji baraka na salamu kwa viongozi wa kanisa na kila mwaamini.
Iliyochaguliwa sasa
Waebrania UTANGULIZI: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.