Hosea 9:1-9
Hosea 9:1-9 BHN
Msifurahi enyi Waisraeli! Msifanye sherehe kama mataifa mengine; maana, mmekuwa wazinzi kwa kumwacha Mungu wenu. Mmefurahia malipo ya uzinzi, kila mahali pa kupuria nafaka. Lakini ngano na mapipa ya divai haitawalisha, hamtapata divai mpya. Hawatakaa katika nchi ya Mwenyezi-Mungu; naam, watu wa Efraimu watarudi utumwani Misri; watakula vyakula najisi huko Ashuru. Hawatamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya divai, wala hawatamfurahisha kwa tambiko zao. Chakula chao kitakuwa kama cha matanga, wote watakaokila watatiwa unajisi. Kitakuwa chakula cha kuwashibisha tu, hakitafaa kuletwa nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu. Mtafanya nini katika sikukuu ile iliyopangwa, au katika karamu ya Mwenyezi-Mungu? Mtakapoyakimbia maangamizi ya nchi yenu, Misri itawakaribisheni kwake, lakini makaburi yenu yawangoja huko Memfisi. Magugu yatamiliki hazina zenu za fedha, miiba itajaa katika mahema yenu. Siku za adhabu zimewadia, naam, siku za kulipiza kisasi zimefika; Waisraeli lazima wautambue wakati huo! Nyinyi mnasema, “Nabii ni mpumbavu; anayeongozwa na roho ni mwendawazimu.” Mnasema hivyo kwa sababu ya uovu wenu mkubwa, kwa sababu ya chuki yenu kali dhidi yake. Nabii ni mlinzi wa Waefraimu kwa niaba ya Mungu; lakini, kokote aendako anategewa mtego kama ndege. Hata nyumbani mwa Mungu wake anachukiwa. Nyinyi mmezama katika uovu, kama ilivyokuwa kule Gibea. Mungu atayakumbuka makosa yao, na kuwaadhibu kwa dhambi zao.