Hosea 9:1-9
Hosea 9:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Usifurahi, Israeli, kwa sababu ya furaha, kama hao mataifa; kwa kuwa umezini juu ya Mungu wako, umependa ujira katika kila sakafu ya nafaka. Sakafu na shinikizo hazitawalisha, na divai mpya itampungukia. Hawatakaa katika nchi ya BWANA; lakini Efraimu atarudi Misri, nao watakula chakula kinajisi katika Ashuru. Hawatammiminia BWANA divai, wala hazitampendeza sadaka zao; mkate wao utakuwa kama chakula cha matanga kwao; wote watakaokila watatiwa unajisi; kwa maana mkate wao utakuwa kwa shauku zao; hautaingia katika nyumba ya BWANA. Mtafanya nini katika siku ya mkutano wa idi, na katika siku ya karamu ya BWANA? Kwa maana, tazama, wamekwenda zao ili kukimbia uharibifu, lakini Misri itawakusanya, Nofu itawazika; vitu vyao vya fedha viwapendezavyo, magugu yatavimiliki; miiba itakuwa katika hema zao. Siku za kupatilizwa zimekuja, siku za kulipa zimefika; Israeli atayajua hayo; huyo nabii ni mpumbavu, huyo mtu mwenye roho ana wazimu; kwa sababu ya wingi wa uovu wako, na kwa sababu uadui umekuwa mkubwa. Efraimu alikuwa mlinzi pamoja na Mungu wangu; na huyo nabii, mtego wa mwinda ndege u katika njia zake zote; katika nyumba ya Mungu wake umo uadui. Wamejiharibu mno, kama katika siku za Gibea; ataukumbuka uovu wao, atazilipiza dhambi zao.
Hosea 9:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Msifurahi enyi Waisraeli! Msifanye sherehe kama mataifa mengine; maana, mmekuwa wazinzi kwa kumwacha Mungu wenu. Mmefurahia malipo ya uzinzi, kila mahali pa kupuria nafaka. Lakini ngano na mapipa ya divai haitawalisha, hamtapata divai mpya. Hawatakaa katika nchi ya Mwenyezi-Mungu; naam, watu wa Efraimu watarudi utumwani Misri; watakula vyakula najisi huko Ashuru. Hawatamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya divai, wala hawatamfurahisha kwa tambiko zao. Chakula chao kitakuwa kama cha matanga, wote watakaokila watatiwa unajisi. Kitakuwa chakula cha kuwashibisha tu, hakitafaa kuletwa nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu. Mtafanya nini katika sikukuu ile iliyopangwa, au katika karamu ya Mwenyezi-Mungu? Mtakapoyakimbia maangamizi ya nchi yenu, Misri itawakaribisheni kwake, lakini makaburi yenu yawangoja huko Memfisi. Magugu yatamiliki hazina zenu za fedha, miiba itajaa katika mahema yenu. Siku za adhabu zimewadia, naam, siku za kulipiza kisasi zimefika; Waisraeli lazima wautambue wakati huo! Nyinyi mnasema, “Nabii ni mpumbavu; anayeongozwa na roho ni mwendawazimu.” Mnasema hivyo kwa sababu ya uovu wenu mkubwa, kwa sababu ya chuki yenu kali dhidi yake. Nabii ni mlinzi wa Waefraimu kwa niaba ya Mungu; lakini, kokote aendako anategewa mtego kama ndege. Hata nyumbani mwa Mungu wake anachukiwa. Nyinyi mmezama katika uovu, kama ilivyokuwa kule Gibea. Mungu atayakumbuka makosa yao, na kuwaadhibu kwa dhambi zao.
Hosea 9:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Usifurahi, Israeli, kwa sababu ya furaha, kama hao mataifa; kwa kuwa umezini juu ya Mungu wako, umependa ujira katika kila sakafu ya nafaka. Sakafu na shinikizo hazitawalisha, na divai mpya itampungukia. Hawatakaa katika nchi ya BWANA; lakini Efraimu atarudi Misri, nao watakula chakula najisi katika Ashuru. Hawatammiminia BWANA divai, wala hazitampendeza sadaka zao; mkate wao utakuwa kama chakula cha matanga kwao; wote watakaokila watatiwa unajisi; kwa maana mkate wao utakuwa kwa shauku zao; hautaingia katika nyumba ya BWANA. Mtafanya nini katika siku ya mkutano wa sikukuu teule, na katika siku ya karamu ya BWANA? Kwa maana, tazama, wamekwenda zao ili kukimbia uharibifu, lakini Misri itawakusanya, Nofu itawazika; vitu vyao vya fedha viwapendezavyo, magugu yatavimiliki; miiba itakuwa katika hema zao. Siku za kupatilizwa zimekuja, siku za kulipa zimefika; Israeli atayajua hayo; huyo nabii ni mpumbavu, huyo mtu mwenye roho ana wazimu; kwa sababu ya wingi wa uovu wako, na kwa sababu uadui umekuwa mkubwa. Efraimu alikuwa mlinzi pamoja na Mungu wangu; na huyo nabii, mtego wa mwindaji ndege u katika njia zake zote; katika nyumba ya Mungu wake umo uadui. Wamejiharibu mno, kama katika siku za Gibea; ataukumbuka uovu wao, atazilipiza dhambi zao.
Hosea 9:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Usifurahie, ee Israeli; usishangilie kama mataifa mengine. Kwa kuwa hukuwa mwaminifu kwa Mungu wako; umependa ujira wa kahaba kwenye kila sakafu ya kupuria nafaka. Sakafu za kupuria nafaka na mashinikizo ya kukamulia divai havitalisha watu, divai mpya itawapungukia. Hawataishi katika nchi ya BWANA, Efraimu atarudi Misri na atakula chakula kilicho najisi huko Ashuru. Hawatammiminia BWANA sadaka ya divai wala dhabihu zao hazitampendeza. Dhabihu kama hizo zitakuwa kwao kama mkate wa waombolezaji; nao wote wazilao watakuwa najisi. Chakula hiki kitakuwa kwa ajili yao wenyewe; kisije katika Hekalu la BWANA. Mtafanya nini katika siku ya sikukuu zenu zilizoamriwa, katika siku za sikukuu za BWANA? Hata ikiwa wataokoka maangamizi, Misri atawakusanya, nayo Memfisi itawazika. Hazina zao za fedha zitasongwa na michongoma, nayo miiba itafunika mahema yao. Siku za adhabu zinakuja, siku za malipo zimewadia. Israeli na afahamu hili. Kwa sababu dhambi zenu ni nyingi sana na uadui wenu ni mkubwa sana, nabii anadhaniwa ni mpumbavu, mtu aliyeongozwa na Mungu anaonekana mwendawazimu. Nabii, pamoja na Mungu wangu, ndiye mlinzi juu ya Efraimu, hata hivyo mitego inamngojea katika mapito yake yote, na uadui katika nyumba ya Mungu wake. Wamezama sana katika rushwa, kama katika siku za Gibea. Mungu atakumbuka uovu wao na kuwaadhibu kwa ajili ya dhambi zao.