Isaya 35
35
Furaha ijayo ya Yerusalemu
1Nyika na nchi kavu vitachangamka,
jangwa litafurahi na kuchanua maua.
2Litachanua maua kwa wingi kama waridi,
litashangilia na kuimba kwa furaha.
Mungu atalijalia fahari ya milima ya Lebanoni,
uzuri wa mlima Karmeli na wa bonde la Sharoni.
Watu watauona utukufu wa Mwenyezi-Mungu,
watauona ukuu wa Mungu wetu.
3 #35:3 Taz Ebr 12:12 Imarisheni mikono yenu dhaifu,
kazeni magoti yenu manyonge.
4Waambieni waliokufa moyo:
“Jipeni moyo, msiogope!
Tazameni Mungu wenu atakuja kulipiza kisasi,
atakuja kuwaadhibu maadui zenu;
atakuja yeye mwenyewe kuwaokoeni.”
5 #35:5-6 Taz Mat 11:5; Luka 7:22 Hapo vipofu wataona tena,
na viziwi watasikia tena.
6Walemavu watarukaruka kama paa,
na bubu wataimba kwa furaha.
Maji yatabubujika nyikani
na vijito vya maji jangwani.
7Mchanga wa moto jangwani utakuwa bwawa la maji,
ardhi kavu itabubujika vijito vya maji.
Makao ya mbwamwitu yatajaa maji;
nyasi zitamea na kukua kama mianzi.
8Humo kutakuwa na barabara kuu,
nayo itaitwa “Njia Takatifu.”
Watu najisi hawatapitia humo,
ila tu watu wake Mungu;
wapumbavu hawatadiriki kuikanyaga,
9humo hakutakuwa na simba,
mnyama yeyote mkali hatapitia humo,
hao hawatapatikana humo.
Lakini waliokombolewa ndio watakaopita humo.
10Waliokombolewa na Mwenyezi-Mungu watarudi,
watakuja Siyoni wakipiga vigelegele.
Watakuwa wenye furaha ya milele,
watajaliwa furaha na shangwe;
huzuni na kilio vitatoweka kabisa.
Iliyochaguliwa sasa
Isaya 35: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.