Yakobo UTANGULIZI
UTANGULIZI
Hatujui kwa hakika ni Yakobo yupi aliyeandika barua hii, ila wengi wanafikiri ni yule Yakobo anayesemwa kwamba ni nduguye Yesu (huyo “ndugu” anatajwa kwa jina katika Marko 6:3). Yakobo anayefahamika zaidi katika jumuiya ya Wakristo kule Yerusalemu alikuwa mwenye wadhifa mkubwa (taz Mate 12:17; 15:13 na 21:18; Gal 1:19 na 2:9). Mwandishi anaonekana kuwa ni mtu mwenye kupenda vitendo: “Msijidanganye wenyewe kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa vitendo” (1:22).
Walengwa wa barua yenyewe sio mtu binafsi au jumuiya fulani moja ya Wakristo, bali ni “makabila kumi na mawili yaliyotawanyika ulimwenguni”, msemo unaotumika kama mfano kuwataja Wakristo waliotawanyika popote duniani.
Barua hii ya Yakobo inafanana na barua katika maneno ya kuanzia tu. Haina alama za barua za nyakati hizo na wala haina salamu za mwisho kama kawaida ya barua nyingine za wakati huo. Si rahisi pia kuonesha muundo kamili wa barua hii ila ni dhahiri mwandishi anatumia vielelezo mbalimbali vyenye uzito maalumu kuyatoa mafundisho yake kuhusu mwongozo unaopaswa kuzingatiwa na watu wanaomwamini Yesu Kristo: Matajiri hawapaswi kujiona afadhali kuliko maskini; haifai kusikiliza bila kutenda yanayotakiwa; kuamini sio jambo la akili tu bali ni vitendo (2:14-26). Mwandishi anashutumu uovu unaotendwa kwa ulimi, yaani maneno (3:1-12). Hekima ya kweli (3:13-18). Mwandishi anawashutumu vikali wale wanaosababisha ugomvi na kuwahukumu wengine; anawaonya matajiri wanaowadhulumu wafanyakazi wao (4:1–5:6) na kwa kumalizia anawataka wasomaji wawe na uvumilivu, wadumu katika kusali.
Iliyochaguliwa sasa
Yakobo UTANGULIZI: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.