Yeremia 13
13
Kikoi cha kitani
1Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Nenda ukajinunulie kikoi cha kitani, ukajifunge kiunoni; lakini usikitie majini.” 2Basi, nikaenda, nikanunua kikoi kama alivyoniagiza Mwenyezi-Mungu, nikajifunga kiunoni. 3Kisha, neno la Mwenyezi-Mungu likanijia mara ya pili: 4“Kichukue kikoi ulichonunua na ambacho umejifunga kiunoni, uende kwenye mto Eufrate na kukificha katika pango mwambani.” 5Basi, nikaenda na kukificha kikoi hicho karibu na mto Eufrate, kama Mwenyezi-Mungu alivyoniamuru.
6Ikawa, baada ya siku nyingi, Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Nenda kwenye mto Eufrate, ukakichukue kile kikoi nilichokuamuru ukifiche huko.” 7Basi, nikaenda kwenye mto Eufrate, nikachimbua na kukitoa kile kikoi mahali nilipokuwa nimekificha. Nilipokitoa, nilishangaa kukiona kuwa kilikuwa kimeharibika kabisa; kilikuwa hakifai tena.
8Ndipo neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: 9“Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Hivi ndivyo nitakavyokiharibu kiburi cha Yuda na kiburi kikubwa cha Yerusalemu. 10Watu hawa waovu wanakataa kusikia maneno yangu, na badala yake wanakuwa wakaidi na kufuata mawazo yao wenyewe. Wanaifuata miungu mingine, wanaitumikia na kuiabudu. Hao watakuwa kama kikoi hiki ambacho hakifai kitu. 11Kama vile kikoi kinavyoshikamana na kiuno cha mtu, ndivyo nilivyowashikamanisha nami watu wa Israeli na watu wa Yuda, ili wajulikane kwa jina langu, wanisifu na kunitukuza. Lakini wao hawakunisikiliza. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Mtungi wa divai na hasira ya Mungu
12Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, aliniambia hivi: “Waambie watu wa Israeli kwamba kila mtungi utajazwa divai. Lakini utakapowaambia hivyo, wao watakujibu hivi: ‘Kwani unadhani sisi hatujui kwamba kila mtungi utajazwa divai?’ 13Nawe utawaambia kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitawalewesha wenyeji wote wa nchi hii; wafalme wanaotawala mahali pa Daudi, makuhani, manabii na wakazi wote wa Yerusalemu. 14Nitawagonganisha wao kwa wao kina baba na watoto. Sitawahurumia, sitawaachia wala sitawarehemu, bali nitawaangamiza.”
Yeremia anaonya juu ya majivuno
15Enyi Waisraeli, sikilizeni kwa makini,
msiwe na majivuno maana Mwenyezi-Mungu anasema nanyi.
16Mtukuzeni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,
kabla hajawaletea giza,
nanyi mkajikwaa miguu kwenye milima ya giza.
Nyinyi mnatazamia mwanga,
lakini anaugeuza kuwa utusitusi
na kuufanya kuwa giza nene.
17Lakini kama msiponisikiliza,
moyo wangu utalia machozi faraghani,
kwa sababu ya kiburi chenu.
Nitalia kwa uchungu na kububujika machozi,
kwa kuwa watu wa Mwenyezi-Mungu wametekwa.
Ujumbe wa Mungu kwa jamii ya kifalme
18Mwambie mfalme na mama yake hivi:
“Shukeni kwenye viti vyenu vya enzi,
maana taji zenu nzuri zimeanguka vichwani mwenu.
19Miji ya Negebu imezingirwa;
hakuna awezaye kufungua malango yake.
Watu wa Yuda wamechukuliwa mateka,
wote kabisa wamepelekwa utumwani.”
20Inua macho yako, ee Yerusalemu!
Tazama! Madui zako waja kutoka kaskazini.
Kundi ulilokabidhiwa liko wapi?
Kundi lako zuri li wapi?
21Utasemaje juu ya wale uliodhani ni rafiki,
wale ambao wewe mwenyewe uliwafundisha,
watakapokushinda na kukutawala?
Je, si utakumbwa na uchungu
kama wa mama anayejifungua?
22Nawe utajiuliza moyoni mwako,
“Kwa nini mambo haya yamenipata?”
Sawa! Kama vazi lako limepandishwa juu,
nawe ukatendewa kwa ukatili mno,
hayo ni matokeo ya makosa yako mengi mno.
23Je, Mwethiopia aweza kubadili rangi yake,
au chui madoadoa yake?
Ikiwezekana, nanyi pia mnaweza kutenda mema,
nyinyi mliozoea kutenda maovu!
24Mwenyezi-Mungu atawatawanya kama makapi
yanayopeperushwa na upepo kutoka jangwani.
25Mwenyezi-Mungu asema:
“Hayo ndiyo yatakayokupata,
ndivyo nilivyoamua kukutenda mimi Mwenyezi-Mungu,
kwa sababu umenisahau mimi,
ukaamini miungu ya uongo.
26Nitalipandisha vazi lako hadi kichwani
na aibu yako yote itaonekana wazi.
27Nimeyaona machukizo yako:
Naam, uzinifu wako na uzembe wako,
na uasherati wako wa kupindukia,
juu ya milima na mashambani.
Ole wako ee Yerusalemu!
Mpaka lini utakaa bila kutakaswa?”
Iliyochaguliwa sasa
Yeremia 13: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.