Yeremia 31
31
Waisraeli wanarudi makwao
1Mwenyezi-Mungu asema: “Wakati utakuja ambapo nitakuwa Mungu wa jamaa zote za Israeli nao watakuwa watu wangu.
2Mimi Mwenyezi-Mungu nasema:
Watu walionusurika kuuawa
niliwaneemesha jangwani.
Wakati Israeli alipotafuta kupumzika,
3mimi Mwenyezi-Mungu nilimtokea kwa mbali.
Nami nimekupenda kwa mapendo ya daima,
kwa hiyo nimeendelea kuwa mwaminifu kwako.
4Nitakujenga upya nawe utajengeka,
ewe Israeli uliye mzuri!
Utazichukua tena ngoma zako
ucheze kwa furaha na shangwe.
5Utapanda tena mizabibu
juu ya milima ya Samaria;
wakulima watapanda mbegu
na kuyafurahia mazao yake!
6Maana siku yaja ambapo mlinzi atapiga mbiu
katika vilima vya Efraimu:
‘Amkeni, twende juu mpaka Siyoni
kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.’”
7Maana Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Imbeni kwa furaha kwa ajili ya Yakobo,
pigeni vigelegele kwa ajili ya taifa kuu,
tangazeni, shangilieni na kusema:
‘Mwenyezi-Mungu na awaokoe watu wake,
amewaletea ukombozi waliobaki wa Israeli!’
8Tazama, nitawaleta kutoka nchi ya kaskazini,
nitawakusanya kutoka miisho ya dunia.
Wote watakuwapo hapo;
hata vipofu na vilema,
wanawake waja wazito na wanaojifungua;
umati mkubwa sana utarudi hapa.
9Watarudi wakiwa wanatoa machozi,
nitawarudisha nikiwafariji;
nitawapitisha kando ya vijito vya maji,
katika njia iliyonyoka ambamo hawatajikwaa;
maana mimi nimekuwa baba wa Israeli,
Efraimu ni mzaliwa wangu wa kwanza.
10Enyi mataifa, sikilizeni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu,
litangazeni katika nchi za mbali,
semeni: ‘Aliyemtawanya Israeli, atamkusanya,
atamtunza kama mchungaji atunzavyo kondoo wake.’
11Maana mimi Mwenyezi-Mungu nimemkomboa Yakobo,
nimemwokoa kutoka kwa wenye nguvu kuliko yeye.
12Watakuja na kuimba kwa sauti juu ya mlima Siyoni,
wataona fahari juu ya wema wangu mimi Mwenyezi-Mungu,
kwa nafaka, divai na mafuta niwapavyo,
kwa kondoo na ng'ombe kadhalika;
maisha yao yatakuwa kama bustani iliyotiliwa maji,
wala hawatadhoofika tena.
13Ndipo wasichana wao watafurahi na kucheza,
vijana na wazee watashangilia kwa furaha.
Nitageuza maombolezo yao kuwa furaha,
nitawafariji na kuwapa furaha badala ya huzuni.
14Nitawashibisha makuhani kwa vinono,
nitawaridhisha watu wangu kwa wema wangu.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Huruma ya Mungu kwa Israeli
15Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Sauti imesikika mjini Rama,
maombolezo na kilio cha uchungu.
Raheli anawalilia watoto wake,
wala hataki kufarijiwa kwa ajili yao,
maana wote hawako tena.
16Sasa, acha kulia,
futa machozi yako,
kwani utapata tuzo kwa kazi yako,
mimi Mwenyezi-Mungu nimesema;
watoto wenu watarudi kutoka nchi ya maadui zenu.
17Yapo matumaini kwa siku zenu zijazo,
mimi Mwenyezi-Mungu nimesema;
kwani watoto wenu watarejea nchini mwao.
18“Nimesikia Efraimu akilalamika:
‘Umenichapa ukanifunza nidhamu,
kwani nilikuwa kama ndama asiyezoea nira.
Unigeuze nami nitakugeukia,
kwani wewe ndiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu.
19Maana baada ya kukuasi, nilitubu,
na baada ya kufunzwa, nilijilaumu,
nikaona haya na kuaibika,
maana lawama za ujana wangu ziliniandama.’
20“Efraimu ni mwanangu mpendwa;
yeye ni mtoto wangu nimpendaye sana.
Ndio maana kila ninapomtisha,
bado naendelea kumkumbuka.
Moyo wangu wamwelekea kwa wema;
hakika nitamhurumia.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
21“Weka alama katika njia zako,
simika vigingi vya kukuongoza,
ikumbuke vema ile njia kuu,
barabara uliyopita ukienda.
Ewe Israeli rudi,
rudi nyumbani katika miji yako.
22Utasitasita mpaka lini
ewe binti usiye mwaminifu?
Maana, mimi nimefanya kitu kipya duniani:
Mwanamke amtafuta mwanamume.”#31:22 mwanamke … mwanamume: Maana katika Kiebrania si dhahiri.
Fanaka siku zijazo
23Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Nitakapowafanikisha tena watu wa Israeli, wao watatangaza tena katika nchi ya Yuda na katika miji yake wakisema:
‘Mwenyezi-Mungu akubariki ewe makao adili,
akubariki ee mlima mtakatifu!’
24“Ndipo watu wa Yuda na miji yake yote, wakulima na wachungaji wanaopitapita na makundi yao, watakaa huko pamoja. 25Waliochoka nitawachangamsha, na walegevu nitawapa nguvu. 26Ndio maana mtu ataweza kusema: ‘Niliamka nikatambua kwamba usingizi wangu ulinifaa sana.’”
27Mwenyezi-Mungu asema: “Tazama, siku zaja ambapo nitaijaza nchi ya Israeli na nchi ya Yuda watu na wanyama kama mkulima asiavyo mbegu. 28Na kadiri nilivyokuwa mwangalifu kuwangoa, kuwabomoa, kuwaangusha, kuwaharibu na kuwatesa, ndivyo nitakavyokuwa mwangalifu kuwapanda na kuwajenga. 29Siku hizo watu hawatasema tena:
‘Wazee walikula zabibu chungu,
na meno ya watoto yakatiwa ganzi.’
30La! Kila mmoja atakufa kwa sababu ya dhambi zake mwenyewe; ni yule tu atakayekula zabibu mbivu ndiye meno yake yatatiwa ganzi.”
31Mwenyezi-Mungu asema: “Siku zaja ambapo nitafanya agano jipya na watu wa Israeli na watu wa Yuda. 32Agano hili halitakuwa kama lile nililofanya na wazee wao nilipowatoa kwa mkono wangu kutoka Misri; agano hilo walilivunja, ingawa mimi nilikuwa Bwana wao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. 33Baada ya siku hizo, nitafanya agano lifuatalo na Waisraeli: Nitaiweka sheria yangu ndani yao, na kuiandika katika mioyo yao. Mimi nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. 34Wala haitawabidi kufundishana na kusema: ‘Mjue Mwenyezi-Mungu’, kwa sababu wote, wadogo kwa wakubwa, watanijua mimi Mungu. Maana nitawasamehe makosa yao, wala sitazikumbuka tena dhambi zao.” 35Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu, ambaye jina lake ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi, aliyepanga jua liangaze mchana, mwezi na nyota vimulike usiku, na aifanyaye bahari iwe na mawimbi: 36Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mimi hulifanya jua liangaze mchana, mwezi na nyota vimulike usiku; pia mimi huitikisa bahari, nayo hutoa mawimbi. Jina langu mimi ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Basi, nami nasema: Kadiri ninavyotegemeza mipango hiyo yote yangu kadiri hiyohiyo Israeli watakavyobaki kuwa watu wangu. 37Kama mbingu zaweza kupimwa, na misingi ya dunia kuchunguzwa, basi, nitawatupilia mbali wazawa wa Israeli, kwa sababu ya mambo yote waliyotenda. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
38Mwenyezi-Mungu asema: “Siku zaja ambapo mji huu wa Yerusalemu utajengwa upya kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu, kutoka mnara wa Hananeli hadi Lango la Pembeni. 39Nayo kamba ya kupimia itanyoshwa moja kwa moja hadi mlima Garebu, kisha itazungushwa hadi Goa. 40Bonde lote walimozikwa wafu na kutupiwa majivu, mashamba yote, mpaka kijito cha Kidroni, mpaka pembe ya lango la Farasi kuelekea mashariki, litakuwa eneo takatifu kwa Mwenyezi-Mungu. Hakuna kitakachoharibiwa humo wala kubomolewa tena milele.”
Iliyochaguliwa sasa
Yeremia 31: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.