Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yobu 24

24
1“Mbona Mungu Mwenye Nguvu haweki wakati maalumu wa hukumu;
au kwa nini wamjuao hawazijui siku hizo zake?
2Watu wanaoondoa alama za mipaka ya mashamba,
na wengine huiba mifugo na kuilisha.
3Huwanyanganya yatima punda wao,
humweka rehani ng'ombe wa mjane.
4Huwasukuma maskini kando ya barabara;
maskini wa dunia hujificha mbele yao.
5Kwa hiyo kama pundamwitu
maskini hutafuta chakula jangwani
wapate chochote cha kuwalisha watoto wao.
6Maskini wanalazimika kuokota mabaki ya mavuno mashambani,
wanaokota katika mashamba ya mizabibu ya waovu.
7Usiku kucha hulala uchi bila nguo
wakati wa baridi hawana cha kujifunikia.
8Wamelowa kwa mvua ya milimani,
hujibanza miambani kujificha wasilowe.
9Wapo na wanaowanyakua watoto yatima vifuani mwa mama yao.
Wengine huwaweka rehani watoto wa maskini.
10Watoto hao hufanywa waende uchi bila nguo,
wakivuna ngano huku njaa imewabana,
11wakiwatengenezea waovu mafuta yao,
au kukamua divai bila hata kuionja.
12Kutoka mjini kilio cha wanaokufa chasikika,
na walioumizwa hupaza sauti kuomba msaada;
lakini Mungu hasikilizi kabisa sala zao.
13“Wapo wengine waovu wasiopenda mwanga,
wasiozifahamu njia za mwanga,
na hawapendi kuzishika njia zake.
14Mwuaji huamka mapema alfajiri,
ili kwenda kuwaua maskini na fukara,
na usiku ukifika, kazi yake ni kuiba.
15Mzinifu naye hungojea giza liingie;
akisema, ‘Hakuna atakayeniona;’
kisha huuficha uso wake kwa nguo.
16Usiku wezi huvunja nyumba,
lakini mchana hujifungia ndani;
wala hawajui kabisa mwanga ni nini.
17Kwao wote giza nene ni mwanga wa asubuhi;
wao ni marafiki wa vitisho vya giza nene.
18“Lakini mwasema:
‘Waovu huchukuliwa haraka na mafuriko ya maji,
makao yao hubaki kuwa nchi iliyolaaniwa;
hakuna aendaye kwenye mashamba yao ya mizabibu.’
19Kama theluji inavyoyeyuka katika joto na ukame
ndivyo Kuzimu kunavyowanyakua waovu.
20Maana mzazi wao huwasahau watu hao,
hakuna atakayewakumbuka tena.
Ndivyo uovu ulivyovunjwa kama mti.
21“Waovu huwadhulumu wanawake wasiopata watoto.
Wala hawawatendei wema wanawake wajane.
22Mungu, kwa nguvu yake huwaangamiza wenye uwezo,
huinuka nao hukata tamaa ya kuishi.
23Huwaacha waovu wajione salama,
lakini macho yake huchunguza mienendo yao.
24Waovu hufana kwa muda tu, kisha hutoweka,
hunyauka na kufifia kama jani,
hukatiliwa mbali kama masuke ya ngano.
25Nani basi, awezaye kuhakikisha kuwa mimi ni mwongo
na kuonesha kwamba maneno yangu si kweli?”

Iliyochaguliwa sasa

Yobu 24: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia