Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yobu 30

30
1“Lakini sasa watu wananidhihaki,
tena watu walio wadogo kuliko mimi;
watu ambao baba zao niliwaona hawafai
hata kuwaangalia mbwa wangu wakilinda kondoo.
2Ningepata faida gani mikononi mwao,
watu ambao nguvu zao zilikuwa zimewaishia?
3Katika ufukara na njaa kali
walitafutatafuta cha kutafuna nyikani#30:3 walitafutatafuta … nyikani: Tafsiri nyingine: Waliguguna huko nyikani.
sehemu tupu zisizokuwa na chakula.
4Walichuma mimea jangwani na majani msituni wakala,
walikula hata mizizi ya mti wa mfagio.
5Walifukuzwa mbali na watu,
watu waliwapigia kelele kama wezi.
6Iliwapasa kutafuta usalama mapangoni,
kwenye mashimo ardhini na miambani.
7Huko vichakani walilia kama wanyama,
walikusanyika pamoja chini ya upupu.
8Walikuwa wapumbavu wakuu na mabaradhuli
ambao walilazimika kufukuzwa nchini kwa kiboko.
9“Na sasa wamenitungia wimbo wa kunizomea,
nimekuwa kitu cha dhihaka kwao.
10Wananichukia na kuniepa;
wakiniona tu wanatema mate.
11Kwa kuwa Mungu amenidhoofisha na kuniaibisha,
wamekuwa huru kunitendea wapendavyo.
12Genge la watu lainuka kunishtaki#30:12 kunishtaki: Au upande wangu wa kulia.
likitafuta kuniangusha kwa kunitegea.
Linanishambulia ili niangamie.
13Watu hao hukata njia yangu
huchochea balaa yangu,
na hapana mtu wa kuwazuia.#30:13 kuwazuia: Kiebrania: Kuwasaidia.
14Wanakuja kama kwenye ufa mkubwa,
na baada ya shambulio wanasonga mbele.
15Hofu kuu imenishika;
hadhi yangu imetoweka kama kwa upepo,
na ufanisi wangu umepita kama wingu.
16“Sasa sina nguvu yoyote nafsini mwangu;
siku za mateso zimenikumba.
17Usiku mifupa yangu yote huuma,
maumivu yanayonitafuna hayapoi.
18Mungu amenikaba kwa mavazi yangu,
amenibana kama ukosi wa shati langu.#30:18 aya hii ni ngumu sana kutafsiri.
19Amenibwaga matopeni;
nimekuwa kama majivu na mavumbi.
20Nakulilia, lakini hunijibu,
nasimama kuomba lakini hunisikilizi.
21Umegeuka kuwa mkatili kwangu,
wanitesa kwa mkono wako wenye nguvu.
22Wanitupa katika upepo na kunipeperusha;
wanisukasuka huku na huko katika dhoruba kali.
23Naam! Najua utanipeleka tu kifoni,
mahali watakapokutana wote waishio.
24“Je, mtu akikumbwa na maangamizi hainui mkono?
Je, mtu akiwa taabuni haombi msaada#30:24 aya hii katika Kiebrania si dhahiri.
25Je, sikuwalilia wale waliokuwa na taabu?
Je, sikuona uchungu kwa ajili ya maskini?
26Lakini nilipotazamia mema, mabaya yalinipata,
nilipongojea mwanga, giza lilikuja.
27Moyo wangu wahangaika wala hautulii kamwe;
siku za mateso zimekumbana nami.
28Napitapita nikiomboleza, kwangu hamna jua.
Nasimama hadharani kuomba msaada.
29Kwa kilio nimekuwa ndugu yake mbwamwitu,
mimi na mbuni hamna tofauti.
30Ngozi yangu imebambuka
mifupa yangu inaungua kwa homa.
31Kinubi changu kimekuwa cha kufanya matanga
filimbi yangu kwa ajili ya kuomboleza.

Iliyochaguliwa sasa

Yobu 30: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia