Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yobu 5

5
1“Ita sasa, uone kama kuna wa kukuitikia.
Ni yupi kati ya watakatifu utakayemwita?
2Ama kweli hangaiko humuua mpumbavu,
na wivu humwangamiza mjinga.
3Nimepata kuona mpumbavu akifana,
lakini ghafla nikayalaani makao yake.
4Watoto wake hawana usalama;
hudhulumiwa mahakamani,#5:4 mahakamani: Neno kwa neno: Langoni palitolewa hukumu.
na hakuna mtu wa kuwatetea.
5Mazao yake huliwa na wenye njaa,
hata nafaka iliyoota kati ya miiba;#5:5 hata … miiba: Maana katika makala ya Kiebrania si dhahiri.
wenye tamaa huuonea shauku utajiri wake.
6Kwa kawaida mateso hayatoki mavumbini
wala matatizo hayachipui udongoni.
7Bali binadamu huzaliwa apate taabu,
kama cheche za moto zirukavyo juu.
8“Kama ningekuwa wewe ningemgeukia Mungu,
ningemwekea yeye Mungu kisa changu,
9yeye atendaye makuu yasiyochunguzika,
atendaye maajabu yasiyohesabika.
10Huinyeshea nchi mvua,
hupeleka maji mashambani.
11Huwainua juu walio wanyonge,
wenye kuomboleza huwapa usalama.
12Huvunja mipango ya wenye hila,
matendo yao yasipate mafanikio.
13 # Taz 1Kor 3:19 Huwanasa wenye hekima kwa werevu wao,
mipango ya wajanja huikomesha mara moja.
14Hao huona giza wakati wa mchana,
adhuhuri hupapasapapasa kama vile usiku.
15Lakini Mungu huwaokoa yatima#5:15 yatima: Maana katika Kiebrania si dhahiri. wasiuawe,
huwanyakua fukara mikononi mwa wenye nguvu.
16Hivyo maskini wanalo tumaini,
nao udhalimu hukomeshwa.
17 # Taz Meth 3:11; Ebr 12:5-6 “Heri mtu yule ambaye Mungu anamrudi!
Hivyo usidharau Mungu Mwenye Nguvu anapokuadhibu.
18 # Taz Hos 6:1 Kwani yeye huumiza na pia huuguza;
hujeruhi, na kwa mkono wake huponya.
19Atakuokoa katika maafa zaidi ya mara moja;
katika balaa la mwisho, uovu hautakugusa.
20Wakati wa njaa atakuokoa na kifo,
katika mapigano makali atakuokoa.
21Utakingwa salama na mashambulio ya ulimi,
wala hutaogopa maangamizi yajapo.
22Maangamizi na njaa vijapo, utacheka,
wala hutawaogopa wanyama wakali wa nchi.
23Nawe utaafikiana na mawe ya shambani,
na wanyama wakali watakuwa na amani nawe.
24Utaona nyumbani mwako mna usalama;
utakagua mifugo yako utaiona yote ipo.
25Utaona pia wazawa wako watakuwa wengi,
wengi kama nyasi mashambani.
26Utafariki ukiwa mkongwe mtimilifu,
kama mganda wa ngano ya kupurwa iliyoiva vizuri.
27Basi huu ndio utafiti wetu; tena ni ukweli;
uusikie na kuuelewa kwa faida yako.”

Iliyochaguliwa sasa

Yobu 5: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia