Yobu UTANGULIZI
UTANGULIZI
Kitabu hiki chaitwa kwa jina la mtu anayehusika zaidi katika habari zake ambaye anakumbana na suala la kuweko kwa “mateso”. Kitabu chenyewe ni kimojawapo cha vitabu vya mfumo wa hekima na mtindo wa kishairi, ambamo wazo la kuishi kwa uadilifu na maana ya maisha ndiyo kitovu chake. Jambo hasa linalokabiliwa ni suala la mateso ya binadamu hapa duniani na jinsi Mungu anavyohusika. Ama kweli kitabu cha Yobu ni kimojawapo cha vitabu vichache vya Agano la Kale chenye maandiko ya ufasaha mkubwa sio tu kwa mfumo wake wa kimaandishi na kishairi bali pia kwa mawazo yake mazitomazito. Tena, miongoni mwa vitabu vya Biblia, labda hiki ni kitabu kigumu kupita vyote.
Katika sehemu ya mwanzo ya kitabu chenyewe ambayo imeandikwa kwa mtindo wa maandishi wa kawaida (sio kishairi wala kwa tenzi), tunahabarishwa juu ya hali ya Yobu. Yeye alikuwa mtu wa nchi ya Usi, tajiri na mcha Mungu. Kwa idhini ya Mungu anajaribiwa na Shetani, akapoteza watoto wake, mali zake zote na kupata ugonjwa mbaya wa ngozi. Katika hali hiyo anatembelewa na rafiki zake ambao walitaka kumfariji. Kisha mwandishi anatupatia mazungumzo kati ya Yobu na rafiki zake, yote katika mashairi. Rafiki za Yobu wanatoa hoja zao kulingana na mapokeo ya kidini: Mungu humtuza mtu mwema na kumwadhibu mwovu. Kwa hiyo mateso ya Yobu yanamaanisha kuwa yeye ametenda dhambi. Kwa upande wa Yobu lakini, hiyo sivyo ilivyo. Yeye hakutenda dhambi; na wala haoni sababu ya Mungu kumweka katika hali hiyo. Jambo la “kuelewa” na “kufahamu” au “kujua” wazo ambalo linachukua nafasi maalumu katika maandishi ya hekima, ndilo linalojitokeza sana katika masimulizi ya Yobu na rafiki zake. Kutokana na hayo, Mungu mwenyewe anamkabili na kumhoji. Mungu anapotoa tamko lake huwa hayajibu masuala ya Yobu ila tu anaonesha ukuu wa umungu wake na hekima yake. Hapo Yobu anakiri ujinga wake kwamba amenena bila kufikiri. Anakiri kwamba Mungu ndiye kweli mweza wa yote.
Mwishoni mwa mashairi hayo, yanafuata maandishi ya kawaida ambamo tunaambiwa kwamba Yobu alirudishiwa hali yake ya mafanikio ya hapo awali, tena maradufu na pia Mungu anawakaripia rafiki zake Yobu kwa kushindwa kuelewa maana ya mateso ya Yobu.
Ni dhahiri kwamba kitabu hiki hakitatui tatizo la mateso ya binadamu. Badala yake panatolewa mitazamo miwili juu ya chanzo cha mateso: Mtazamo wa kwanza unaoshikiliwa na Elifazi, Bildadi na Zofari; na mtazamo mwingine tofauti unashikiliwa na Yobu.
Iliyochaguliwa sasa
Yobu UTANGULIZI: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.