Luka 19:41-48
Luka 19:41-48 BHN
Alipokaribia zaidi na kuuona ule mji, Yesu aliulilia akisema: “Laiti ungelijua leo hii mambo yaletayo amani! Lakini sasa yamefichika machoni pako. Maana siku zaja ambapo adui zako watakuzungushia maboma, watakuzingira na kukusonga pande zote. Watakupondaponda wewe pamoja na watoto wako ndani ya kuta zako; hawatakuachia hata jiwe moja juu ya jingine, kwa sababu hukuutambua wakati Mungu alipokujia kukuokoa.” Kisha, Yesu aliingia hekaluni, akaanza kuwafukuza nje wafanyabiashara akisema, “Imeandikwa: ‘Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala’; lakini nyinyi mmeifanya kuwa pango la wanyanganyi.” Yesu akawa anafundisha kila siku hekaluni. Makuhani wakuu, waalimu wa sheria na viongozi wa watu walitaka kumwangamiza, lakini hawakuwa na la kufanya, maana watu wote walikuwa wakimsikiliza kwa makini kabisa.