Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 20:1-8

Luka 20:1-8 BHN

Siku moja, Yesu alipokuwa akiwafundisha watu hekaluni na kuwahubiria juu ya Habari Njema, makuhani wakuu na waalimu wa sheria pamoja na wazee walifika, wakasema, “Tuambie! Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani?” Yesu akawaambia, “Na mimi nitawaulizeni swali: Mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka kwa Mungu au kwa watu?” Lakini wao wakajadiliana hivi: “Tukisema yalitoka kwa Mungu, yeye atatuuliza: ‘Mbona hamkumsadiki?’ Na tukisema yalitoka kwa binadamu, watu wote hapa watatupiga mawe, maana wote wanaamini kwamba Yohane alikuwa nabii.” Basi, wakamwambia, “Hatujui mamlaka hayo yalitoka wapi.” Yesu akawaambia, “Hata mimi sitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.”