Mathayo 11:16-24
Mathayo 11:16-24 BHN
“Basi, nitakifananisha kizazi hiki na kitu gani? Ni kama vijana waliokuwa wamekaa uwanjani, wakawa wakiambiana kikundi kimoja kwa kingine: ‘Tumewapigieni ngoma lakini hamkucheza! Tumeimba nyimbo za huzuni lakini hamkuomboleza!’ Kwa maana Yohane alikuja, akafunga na wala hakunywa divai, nao wakasema: ‘Amepagawa na pepo’. Mwana wa Mtu akaja, anakula na kunywa, nao wakasema: ‘Mwangalieni huyu, mlafi na mlevi, rafiki yao watozaushuru na wenye dhambi!’ Hata hivyo, hekima ya Mungu inathibitishwa kuwa njema kutokana na matendo yake.” Kisha Yesu akaanza kuilaumu miji ambayo, ingawaje alifanya miujiza mingi humo, watu wake hawakutaka kutubu: “Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwisha vaa mavazi ya gunia kitambo na kujipaka majivu kutubu. Hata hivyo, nawaambieni, siku ya hukumu, nyinyi mtapata adhabu kubwa kuliko ya Tiro na Sidoni. Na wewe Kafarnaumu, je, utajikweza mpaka mbinguni? Utaporomoshwa mpaka kuzimu! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika kule Sodoma, mji huo ungalikuwako mpaka hivi leo. Lakini nawaambieni, siku ya hukumu wewe utapata adhabu kubwa kuliko ya Sodoma.”