Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 13:47-58

Mathayo 13:47-58 BHN

“Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na wavu uliotupwa baharini, ukanasa samaki wa kila aina. Ulipojaa, watu waliuvuta pwani, wakaketi, wakachagua samaki wazuri wakawaweka ndani ya vikapu vyao, na wabaya wakawatupa. Ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati: Malaika watatokea, watawatenganisha watu wabaya na watu wema, na kuwatupa hao wabaya katika tanuri ya moto. Huko watalia na kusaga meno.” Yesu akawauliza, “Je, mmeelewa mambo haya yote?” Wakamjibu, “Naam.” Naye akawaambia, “Hivyo basi, kila mwalimu wa sheria anayekuwa mwanafunzi wa ufalme wa mbinguni anafanana na mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.” Yesu alipomaliza kusema mifano hiyo alitoka mahali hapo, akaenda kijijini kwake. Huko akawa anawafundisha watu katika sunagogi lao hata wakashangaa, wakasema, “Huyu amepata wapi hekima hii na maajabu? Je, huyu si yule mwana wa seremala? Je, mama yake si anaitwa Maria, na ndugu zake si kina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda? Na dada zake je, si wote wako hapa pamoja nasi? Basi, amepata wapi haya yote?” Basi, wakawa na mashaka naye. Lakini Yesu akawaambia, “Nabii hakosi kuheshimiwa, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani mwake!” Kwa hiyo, hakutenda miujiza mingi pale kwa sababu ya kutoamini kwao.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mathayo 13:47-58