Marko 12:38-44
Marko 12:38-44 BHN
Katika mafundisho yake, Yesu alisema, “Jihadharini na waalimu wa sheria ambao hupenda kupitapita wamejivalia kanzu ndefu na kusalimiwa na watu kwa heshima sokoni; hupenda kuketi mahali pa heshima katika masunagogi, na kuchukua nafasi za heshima katika karamu. Huwadhulumu wajane huku wakijisingizia kusali sala ndefu! Siku ya hukumu watapata adhabu kali.” Yesu alikuwa ameketi karibu na sanduku la hazina. Akawa anatazama jinsi watu wengi walivyokuwa wakitoa fedha na kuzitia katika hazina ya hekalu. Matajiri wengi walitoa fedha nyingi. Hapo akaja mama mmoja mjane maskini, akatoa sarafu mbili ndogo za fedha. Hapo Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Kweli nawaambieni, mama huyu mjane maskini ametia katika sanduku la hazina kiasi kikubwa kuliko walichotia wengine wote. Maana wengine wote walitoa kutokana na ziada ya mali zao, lakini huyu mama, ingawa ni maskini, ametoa yote aliyokuwa nayo, ametoa kila kitu alichohitaji kwa kuishi.”