Marko 5:1-20
Marko 5:1-20 BHN
Basi, wakafika katika nchi ya Wagerase, ngambo ya ziwa. Mara tu Yesu aliposhuka mashuani, mtu mmoja aliyepagawa na pepo mchafu alitoka makaburini, akakutana naye. Mtu huyo alikuwa akiishi makaburini wala hakuna mtu aliyeweza tena kumfunga kwa minyororo. Mara nyingi walimfunga kwa pingu na minyororo lakini kila mara aliweza kuikata hiyo minyororo na kuzivunja hizo pingu, wala hakuna mtu aliyeweza kumzuia. Mchana na usiku alikaa makaburini na milimani akipaza sauti na kujikatakata kwa mawe. Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia, akamwinamia akisema kwa sauti kubwa, “Una nini nami, wewe Yesu Mwana wa Mungu aliye juu? Kwa jina la Mungu, nakusihi usinitese!” ( Alisema hivyo kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia, “Pepo mchafu, mtoke mtu huyu.”) Basi, Yesu akamwuliza, “Jina lako nani?” Naye akajibu, “Jina langu ni ‘Jeshi,’ maana sisi tu wengi.” Kisha akamsihi Yesu asiwafukuze hao pepo katika nchi ile. Kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe malishoni kwenye mteremko wa mlima. Basi, hao pepo wakamsihi, “Utupeleke kwa hao nguruwe, tuwaingie.” Naye akawaruhusu. Basi, hao pepo wachafu wakatoka, wakawaingia wale nguruwe. Kundi lote la nguruwe wapatao 2,000 likaporomoka kwenye ule mteremko mkali mpaka ziwani, likatumbukia majini. Wachungaji wa hao nguruwe walikimbia, wakatangaza jambo hilo mjini na mashambani. Watu wakafika kuona yaliyotukia. Wakamwendea Yesu, wakamwona na mtu yuleyule aliyekuwa amepagawa na jeshi la pepo ameketi chini, amevaa nguo na ana akili yake sawa, wakaogopa. Watu walioshuhudia tukio hilo wakawaeleza wengine mambo yaliyompata huyo mtu aliyekuwa amepagawa na pepo na juu ya wale nguruwe. Basi, wakaanza kumwomba aondoke katika nchi yao. Yesu alipokuwa anapanda mashuani, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo akamwomba amruhusu kwenda naye. Lakini Yesu akamkatalia. Badala yake akamwambia, “Nenda nyumbani kwa jamaa yako, ukawaambie mambo yote Bwana aliyokutendea na jinsi alivyokuonea huruma.” Basi, huyo mtu akaenda, akaanza kutangaza huko Dekapoli mambo yote Yesu aliyomtendea; watu wote wakashangaa.