Marko 6:7-13
Marko 6:7-13 BHN
Aliwaita wale wanafunzi kumi na wawili, akaanza kuwatuma wawiliwawili. Aliwapa uwezo wa kuwafukuza pepo wachafu; akawaamuru: “Msichukue chochote mnapokwenda isipokuwa fimbo tu. Msichukue mkate, wala mkoba, wala fedha kibindoni. Vaeni viatu lakini msichukue koti la ziada.” Tena aliwaambia, “Popote mtakapokaribishwa nyumbani, kaeni humo mpaka mtakapoondoka mahali hapo. Mahali popote ambapo watu watakataa kuwakaribisheni au kuwasikiliza, ondokeni hapo na kuyakunguta mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao.” Basi, wakaondoka, wakahubiri watu watubu. Waliwafukuza pepo wengi wabaya; wakawapaka mafuta wagonjwa wengi, wakawaponya.