Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Methali 15

15
1Kujibu kwa upole hutuliza hasira,
lakini neno kali huchochea hasira.
2Ulimi wa mwenye hekima hueneza maarifa,
lakini watu wapumbavu hububujika upuuzi.
3Macho ya Mwenyezi-Mungu huona kila kitu,
humchunguza mtu mwema na mtu mbaya.
4Ulimi mpole ni chanzo cha uhai,
lakini uovu wake huvunja moyo.
5Mpumbavu hudharau mafundisho ya baba yake,
lakini anayekubali maonyo ana busara.
6Nyumbani mwa mwadilifu mna wingi wa mali,
lakini mapato ya waovu huishia na balaa.
7Mdomo wa mwenye hekima hueneza maarifa,
lakini sivyo ilivyo mioyo ya wapumbavu.
8Sadaka ya waovu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu,
lakini sala ya wanyofu humfurahisha Mungu.
9Mwenendo wa waovu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu,
lakini Mungu huwapenda wale wafuatao mambo adili.
10Adhabu kali ipo kwa wanaoacha mwenendo mwema;
yeyote achukiaye kuonywa atakufa.
11Ikiwa Mwenyezi-Mungu ajua yaliyo Kuzimu na Abadoni,
mawazo ya binadamu yatawezaje kujificha mbele yake?
12Mwenye madharau hapendi kuonywa,
hatafuti kamwe maoni ya wenye busara.
13Moyo wa furaha hungarisha uso,
lakini uchungu huvunja moyo.
14Mwenye busara hutafuta maarifa,
lakini wapumbavu hujilisha upuuzi.
15Kwa mnyonge kila siku ni mbaya,
lakini kwa mwenye moyo mchangamfu ni sikukuu.
16Afadhali kuwa na kidogo na kumcha Mwenyezi-Mungu,
kuliko kuwa na mali nyingi pamoja na taabu.
17Afadhali mlo wa jioni wa mchicha na upendo,
kuliko karamu ya nyama nono pamoja na chuki.
18Mtu wa hasira mbaya husababisha ugomvi,
lakini asiye mwepesi wa hasira hutuliza ugomvi.
19Njia ya mvivu imesambaa miiba,
njia ya mwaminifu ni wazi kama barabara kuu.
20Mtoto mwenye hekima humfurahisha baba yake,
lakini mpumbavu humdharau mama yake.
21Upumbavu ni furaha kwa mtu asiye na akili,
lakini mwenye busara huchagua njia iliyo sawa.
22Mipango huharibika kwa kukosa shauri,
lakini kwa washauri wengi, hufaulu.
23Kutoa jibu sahihi hufurahisha;
neno lifaalo kwa wakati wake ni jema mno!
24Njia ya mwenye hekima huelekea juu kwenye uhai,
ili aepe kuingia chini kuzimu.
25Mwenyezi-Mungu huyabomoa makao ya wenye kiburi,
lakini huilinda mipaka ya makao ya mjane.
26Mawazo ya mwovu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu,
bali maneno mema humfurahisha.
27Anayetamani faida ya ulanguzi
anaitaabisha jamaa yake,
lakini achukiaye hongo ataishi.
28Moyo wa mwadilifu hufikiri kabla ya kujibu,
lakini kinywa cha mwovu hububujika uovu.
29Mwenyezi-Mungu yuko mbali na watu waovu,
lakini yu karibu na watu wema kuwasikiliza.
30Macho ya huruma hufurahisha moyo,
habari njema huuburudisha mwili.
31Mtu ambaye husikiliza maonyo mema,
anayo nafasi yake miongoni mwa wenye hekima.
32Anayekataa kufundishwa anajidharau mwenyewe,
bali anayekubali maonyo hupata busara.
33Kumcha Mwenyezi-Mungu ni shule ya hekima;
kabla ya kuheshimika ni lazima kuwa mnyenyekevu.

Iliyochaguliwa sasa

Methali 15: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia