Methali 21
21
1Moyo wa mfalme ni kama maji yanayotiririka;
Mwenyezi-Mungu, huuongoza popote apendapo.
2Matendo yote ya mtu ni sawa machoni pake,
lakini Mwenyezi-Mungu hupima mioyo.
3Kutenda mambo mema na ya haki,
humpendeza Mwenyezi-Mungu kuliko tambiko.
4Macho ya kiburi na moyo wa majivuno
huonesha wazi dhambi ya waovu.
5Mipango ya mtu wa bidii huleta mali kwa wingi,
lakini kila aliye na pupa huishia patupu.
6Mali ipatikanayo kwa udanganyifu,
ni mvuke upitao na mtego wa kifo.
7Ukatili wa wakatili utawafutilia mbali,
maana wanakataa kutenda yaliyo ya haki.
8Njia ya mtu mwenye hatia imepotoka,
lakini mwenendo wa mnyofu umenyooka.
9Afadhali kuishi pembeni juu ya paa,
kuliko kuishi nyumbani na mwanamke mgomvi.
10Anachopania kutenda mtu mbaya ni uovu;
hata kwa jirani yake hana huruma.
11Ukimwadhibu mwenye dhihaka, mjinga hupata hekima;
ukimfundisha mwenye hekima, unampatia maarifa.
12Mungu Mwadilifu#21:12 Mungu Mwadilifu:Mungu. anajua wanayotenda waovu nyumbani kwao;
naye atawaangusha na kuwaangamiza.
13Anayekataa kusikiliza kilio cha maskini,
naye pia hatasikilizwa atakapolilia msaada.
14Hasira hutulizwa kwa zawadi ya siri;
tunu apewayo mtu imefichwa hupooza ghadhabu.
15Haki ikitekelezwa watu wema hufurahi,
lakini watu waovu hufadhaishwa.
16Anayetangatanga mbali na njia ya busara,
atajikuta ametua miongoni mwa wafu.
17Anayependa anasa atakuwa maskini;
anayefikiria tu kula na kunywa hatatajirika.
18Mwovu atapata pigo ambalo halitampata mtu mwema,
mkosefu ataadhibiwa badala ya mnyofu.
19Afadhali kuishi jangwani,
kuliko kukaa na mwanamke mgomvi na msumbufu.
20Nyumbani kwa mwenye busara mna hazina za thamani,
lakini mpumbavu huponda mali yake yote.
21Anayepania uadilifu na huruma,
ataishi maisha marefu na kuheshimiwa.
22Mwenye hekima aweza kuteka mji wa wenye nguvu,
na kuziporomosha ngome wanazozitegemea.
23Achungaye mdomo wake na ulimi wake,
hujiepusha na matatizo.
24Mwenye majivuno na kiburi jina lake ni “Madharau;”
matendo yake yamejaa majivuno ya ufidhuli wake.
25Mvivu hufa kwa kutotimizwa tamaa zake,
maana mikono yake milegevu haitaki kufanya kazi.
26Mchana kutwa mwovu hutamani kupata kitu,
lakini mwadilifu hutoa, tena kwa ukarimu.
27Tambiko ya mwovu ni kitu cha kuchukiza,
huchukiza zaidi akiitoa kwa nia mbaya.
28Shahidi mwongo ataangamia,
lakini msikivu hawezi kunyamazishwa.
29Mtu mwovu hujionesha kuwa jasiri,
lakini mwadilifu huhakikisha ametenda sawa.
30Hakuna hekima, maarifa, wala mawaidha yoyote ya mtu,
yawezayo kumshinda Mwenyezi-Mungu.
31Farasi hutayarishwa kwa vita,
lakini ushindi wamtegemea Mwenyezi-Mungu.
Iliyochaguliwa sasa
Methali 21: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.