Methali 29
29
1Anayeonywa mara nyingi akawa mkaidi,
ataangamia ghafla asipone tena.
2Waadilifu wakitawala watu hufurahi,
lakini waovu wakitawala watu hulalamika.
3Apendaye hekima humfurahisha baba yake;
lakini aandamanaye na malaya hufuja mali yake.
4Mfalme akitumia haki huipatia nchi uthabiti,
lakini akipenda hongo taifa huangamia.
5Mwenye kumbembeleza jirani yake,
anatega mtego wa kujinasa mwenyewe.
6Mtu mbaya hunaswa kwa kosa lake,
lakini mtu mwadilifu huimba na kufurahi.
7Mwadilifu anajua haki za maskini,
lakini mtu mwovu hajui mambo hayo.
8Wenye dharau huutia vurugu mji mzima,
lakini wenye hekima hutuliza ghadhabu.
9Mwenye hekima akibishana na mpumbavu,
mpumbavu huwaka hasira na kucheka bila kutulia.
10Wapendao kumwaga damu humchukia mtu asiye na hatia,
lakini watu wema huyalinda maisha yake.
11Mpumbavu huonesha hasira yake wazi,
lakini mwenye hekima huizuia na kuituliza.
12Mtawala akisikiliza mambo ya uongo,
maofisa wake wote watakuwa waovu.
13Maskini na mkandamizaji wanafanana kwa kitu kimoja:
Wote wawili wamepewa macho na Mwenyezi-Mungu.
14Mfalme anayewaamua maskini kwa haki,
atauona utawala wake umeimarika milele.
15Adhabu na maonyo huleta hekima,
lakini mtoto aliyeachwa afanye apendavyo humwaibisha mama yake.
16Waovu wakitawala maovu huongezeka,
lakini waadilifu watashuhudia kuanguka kwao.
17Mpe nidhamu mwanao naye hatakupa wasiwasi;
yeye ataufurahisha moyo wako.
18Pasipo maono ya kinabii watu hukosa nidhamu;
heri mtu yule anayeshika sheria.
19Mtumwa haonyeki kwa maneno matupu,
maana ingawa anayaelewa yeye hatayatii.
20Wamwona mtu apayukaye bila kufikiri?
Mtu mpumbavu ni afadhali kuliko yeye.
21Ambembelezaye mtumwa wake tangu utoto,
mwishowe mtumwa huyo atamrithi.#29:21 mwishowe … atamrithi: Au Mwishowe mtumwa huyo atakataa kumtii.
22Mwenye ghadhabu huchochea ugomvi,
mtu wa hasira husababisha makosa mengi.
23Kiburi cha mtu humporomosha mwenyewe,
lakini mnyenyekevu wa roho atapata heshima.
24Anayeshirikiana na mwizi anajidhuru mwenyewe;
husikia laana ya aliyeonewa bila kusema neno.
25Kuwaogopa watu ni kujitega mwenyewe,
lakini anayemtumaini Mwenyezi-Mungu yu salama.
26Wengi hupenda kujipendekeza kwa mtawala,
hali mtu hupata haki yake kwa Mwenyezi-Mungu.
27Mdhalimu ni chukizo kwa mnyofu,
naye mnyofu ni chukizo kwa mwovu.
Iliyochaguliwa sasa
Methali 29: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.