Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Methali 6:1-19

Methali 6:1-19 BHN

Mwanangu, kama umejitolea kumdhamini jirani yako, ikiwa umetoa ahadi yako kwa ajili ya mtu huyo, umejibana kwa maneno yako mwenyewe, umejinasa kwa ahadi uliyofanya. Ujue kwamba uko chini ya mamlaka ya mwenzio, lakini mwanangu, ukitaka kujiokoa, basi fanya hivi: Mwendee mtu huyo mara moja umsihi akupe uhuru wako. Jitahidi usiache macho yako yapate usingizi, wala kope za macho yako zisinzie. Jiokoe kwa kujitoa katika mtego huo, mithili ya paa ama ndege amtorokavyo mwindaji. Ewe mvivu! Hebu ukamchungulie sisimizi, fikiria namna yake ya kuishi ukapate hekima. Sisimizi hana kiongozi, ofisa, wala mtawala; lakini hujiwekea chakula wakati wa kiangazi, hujikusanyia akiba wakati wa mavuno. Ewe mvivu, utalala hapo mpaka lini? Utaamka lini katika usingizi wako? Wasema: “Acha nilale kidogo tu, acha nisinzie kidogo! Niache nikunje mikono nipumzike kidogo!” Wakati huo umaskini utakuvamia kama mnyanganyi, ufukara utakufuata kama jambazi. Mtu mwovu, mtu asiyefaa kitu, huzururazurura akisema maneno mapotovu. Hukonyeza jicho kuwakosesha wengine, huparuza kwa nyayo, na kuashiria watu kwa vidole. Akiwa amejaa ulaghai moyoni hutunga maovu, huzusha ugomvi kila mahali. Kutokana na hayo maafa yatamvamia ghafla, ghafla atadhurika vibaya asiweze kupona tena. Kuna vitu sita anavyochukia Mwenyezi-Mungu; naam, vitu saba ambavyo ni chukizo kwake: Macho ya kiburi, ulimi mdanganyifu, mikono inayoua wasio na hatia, moyo unaopanga mipango miovu, miguu iliyo mbioni kutenda maovu, shahidi wa uongo abubujikaye uongo, na mtu achocheaye fitina kati ya ndugu.

Soma Methali 6