Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 107

107
KITABU CHA TANO
(Zaburi 107–150)
Sifa kwa Mungu mwema
1 # Taz Zab 100:5; 106:1; 118:1; 136:1 Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema;
kwa maana fadhili zake zadumu milele!
2Semeni hivyo, enyi mliokombolewa na Mwenyezi-Mungu,
watu ambao aliwaokoa katika taabu,
3akawakusanyeni kutoka nchi za kigeni:
Kutoka mashariki na magharibi,
kutoka kaskazini na kusini.#107:3 kusini: Kiebrania: Bahari; yaani magharibi.
4Baadhi walitangatanga katika jangwa tupu,
wasiweze kufikia mji wa kukaa.
5Waliona njaa na kiu;
wakavunjika moyo kabisa.
6Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu,
naye akawaokoa katika mateso yao.
7Aliwaongoza katika njia iliyonyoka,
mpaka wakaufikia mji wa kukaa.
8Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake;
kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu.
9Yeye huwatosheleza walio na kiu;
na wenye njaa huwashibisha mema.
10Baadhi waliishi katika giza na ukiwa,
wafungwa katika mateso na minyororo,
11kwa sababu waliasi maagizo ya Mungu,
na kuyapuuza mashauri yake Mungu Mkuu.
12Walikuwa hoi kwa kazi ngumu,
wakaanguka chini, pasiwe na wa kuwasaidia.
13Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu,
naye akawaokoa katika mateso yao.
14Aliwatoa katika giza na ukiwa,
na minyororo yao akaivunjavunja.
15Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, kwa fadhili zake;
kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu.
16Yeye huvunja na kufungua milango ya shaba,
na kukatakata fito za chuma.
17Baadhi walipumbaa kwa sababu ya dhambi zao,
waliteseka kwa sababu ya uovu wao;
18chakula kikawa kinyaa kwao,
wakawa nusura wafe.
19Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu,
naye akawaokoa katika mateso yao.
20Kwa neno lake aliwaponya,
akawaokoa wasiangamie.
21Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake;
kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu.
22Wamtolee tambiko za shukrani;
wasimulie matendo yake kwa nyimbo za shangwe.
23Baadhi walisafiri baharini kwa meli,
na kufanya shughuli zao humo baharini.
24Waliyaona matendo ya Mwenyezi-Mungu,
mambo ya ajabu aliyotenda huko.
25Aliamuru, akazusha dhoruba kali,
ikarusha juu mawimbi ya bahari.
26Walitupwa juu angani, kisha chini vilindini;
uhodari wao ukawaishia katika mkasa huo.
27Waliyumbayumba na kupepesuka kama walevi;
maarifa yao ya uanamaji yakawaishia.
28Ndipo katika taabu zao wakamlilia Mwenyezi-Mungu,
naye akawaokoa katika mateso zao.
29Aliifanya ile dhoruba kali itulie,
nayo mawimbi yakanyamaza.
30Hapo wakafurahi kwa kupata utulivu;
akawafikisha kwenye bandari waliyoiendea.
31Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake;
kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu.
32Mtukuzeni katika kusanyiko la watu,
na kumsifu katika baraza la wazee.
33Mungu aliigeuza mito kuwa jangwa,
chemchemi akazikausha kabisa.
34Ardhi yenye rutuba akaifanya udongo wa chumvi,
kwa sababu ya uovu wa wakazi wake.
35Aligeuza majangwa kuwa mabwawa ya maji,
na nchi kame kuwa chemchemi za maji.
36Akawahamishia huko wenye njaa,
nao wakajenga mji wa kukalika.
37Walilima mashamba na kupanda mizabibu,
wakavuna mazao kwa wingi.
38Aliwabariki watu wake, wakaongezeka;
na idadi ya wanyama wao akaizidisha.
39Kisha walipopungua na kuwa wanyonge,
kwa kukandamizwa, kuteswa na huzuni,
40aliwadharau wakuu waliowatesa,
akawazungusha jangwani kusiko na njia.
41Lakini aliwaokoa wahitaji katika taabu zao,
akaongeza jamaa zao kama kundi la kondoo.
42Waadilifu waonapo jambo hilo wanafurahi,
lakini waovu wote wananyamazishwa.
43Wenye hekima na wayafikirie mambo haya,
wazitambue fadhili zake Mwenyezi-Mungu.

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 107: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia