Zaburi 34:1-10
Zaburi 34:1-10 BHN
Nitamtukuza Mwenyezi-Mungu nyakati zote, sitaacha kamwe kuzitamka sifa zake. Mimi nitaona fahari juu ya Mwenyezi-Mungu, wanyonge wasikie na kufurahi. Mtukuzeni Mwenyezi-Mungu pamoja nami, sote pamoja tulisifu jina lake. Nilimwomba Mwenyezi-Mungu naye akanijibu, na kuniondoa katika hofu zangu zote. Mgeukieni Mungu mpate kufurahi; nanyi hamtaaibishwa kamwe. Maskini alimlilia Mwenyezi-Mungu, naye akamsikia, na kumwokoa katika taabu zake zote. Malaika wa Mwenyezi-Mungu huwalinda wote wamchao, na kuwaokoa katika hatari. Jaribuni mwone Mwenyezi-Mungu alivyo mwema. Heri mtu anayekimbilia usalama kwake. Mcheni Mwenyezi-Mungu enyi watakatifu wake; maana wenye kumcha hawatindikiwi na kitu. Hata wanasimba hutindikiwa na kuona njaa; lakini wanaomtafuta Mwenyezi-Mungu hawakosi chochote chema.