Zaburi 51
51
Kuomba msamaha
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi baada ya kukemewa na nabii Nathani kwa kosa lake na Bathsheba)
1Nihurumie, Ee Mungu,
kadiri ya fadhili zako;
ufutilie mbali makosa yangu,
kadiri ya wingi wa huruma yako.
2Unioshe kabisa hatia yangu;
unisafishe dhambi yangu.
3Nakiri kabisa makosa yangu,
daima naiona waziwazi dhambi yangu.
4 # Taz Rom 3:4 Nimekukosea wewe peke yako,
nimetenda yaliyo mabaya mbele yako.
Uamuzi wako ni wa haki
hukumu yako haina lawama.
5Mimi ni mkosefu tangu kuzaliwa kwangu,
mwenye dhambi tangu tumboni mwa mama yangu.
6Wewe wataka unyofu wa ndani;
hivyo nifundishe hekima moyoni.
7Unitakase kwa husopo,#51:7 Husopo: Husopo ni jina la mmea mmoja wa majani madogo laini ambao ulitumiwa katika ibada za kutakasa. nitakate;
unioshe niwe mweupe pe.
8Nijaze furaha na shangwe,
nifurahishe tena, mimi ambaye uliniponda.
9Ugeuke, usiziangalie dhambi zangu;
uzifute hatia zangu zote.
10Uniumbie moyo safi, ee Mungu,
uweke ndani yangu roho mpya na thabiti.
11Usinitupe mbali nawe;
usiniondolee roho yako takatifu.
12Unifanye nifurahi tena kwa kuniokoa,
utegemeze ndani yangu moyo wa utii.
13Hapo nitawafunza wakosefu njia yako,
nao wenye dhambi watarudi kwako.
14Uniokoe na hatia ya umwagaji damu,
ee Mungu, Mungu mwokozi wangu,
nami nitaimba kwa sauti kuwa umeniokoa.
15Uniwezeshe kusema, ee Bwana,
midomo yangu itangaze sifa zako.
16Kwa kweli wewe hupendezwi na tambiko,
ama sivyo mimi ningalikutolea.
Wewe huna haja na tambiko za kuteketezwa.
17tambiko yangu kwako ee Mungu, ni moyo mnyofu;
wewe, ee Mungu, hukatai moyo mnyofu na mtiifu.
18Ee Mungu, upende kuutendea mema mji wa Siyoni;
uzijenge tena upya kuta za mji wa Yerusalemu.
19Hapo utapendezwa na tambiko za kweli:
Sadaka za kuteketezwa na za kuteketezwa nzima;
mafahali watatolewa tambiko madhabahuni pako.
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 51: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.