Zaburi 62:1-12
Zaburi 62:1-12 BHN
Namngojea Mungu peke yake kwa utulivu, kwake watoka wokovu wangu. Yeye peke yake ndiye mwamba na wokovu wangu, yeye ni ngome yangu, sitatikisika. Hata lini mtanishambulia mimi? Hata lini nyinyi nyote mtanipiga, mimi niliye kama kiambaza kilichoinama, kama ukuta unaoanza kubomoka? Mmepanga kuniangusha toka mahali pangu pa heshima; furaha yenu ni kusema uongo. Kwa maneno, mnabariki, lakini moyoni mnalaani. Namngojea Mungu peke yake kwa utulivu; kwake naliweka tumaini langu. Yeye peke yake ndiye mwamba na wokovu wangu, yeye ni ngome yangu, sitatikisika. Wokovu na fahari yangu vyatoka kwa Mungu; mwamba wangu mkuu na kimbilio langu ni Mungu. Enyi watu, mtumainieni Mungu daima; mfungulieni Bwana yaliyo moyoni mwenu. Mungu ndiye kimbilio la usalama wetu. Binadamu wote ni kama pumzi tu; wote, wakubwa kwa wadogo, hawafai kitu. Tena ukiwapima uzito hawafikii kilo, wote pamoja ni wepesi kuliko pumzi. Msitegemee dhuluma, msijisifie mali ya wizi; kama mali zikiongezeka, msizitegemee. Mungu ametamka mara moja, nami nimesikia tena na tena: Kwamba enzi ni mali yake Mungu; naam, nazo fadhili ni zake Bwana; humlipa kila mtu kadiri ya matendo yake.