Zaburi 91:9-16
Zaburi 91:9-16 BHN
Wewe umemfanya Mwenyezi-Mungu kuwa kimbilio lako; naam, Mungu aliye juu kuwa kinga yako. Kwa hiyo, hutapatwa na maafa yoyote; nyumba yako haitakaribiwa na baa lolote. Maana Mungu atawaamuru malaika zake, wakulinde popote uendapo. Watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe. Utakanyaga simba na nyoka, utawaponda wana simba na majoka. Mungu asema: “Nitamwokoa yule anipendaye; nitamlinda anayenitambua! Akiniita, mimi nitamwitikia; akiwa taabuni nitakuwa naye; nitamwokoa na kumpa heshima. Nitamridhisha kwa maisha marefu, nitamjalia wokovu wangu.”