Zaburi 91:9-16
Zaburi 91:9-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Wewe umemfanya Mwenyezi-Mungu kuwa kimbilio lako; naam, Mungu aliye juu kuwa kinga yako. Kwa hiyo, hutapatwa na maafa yoyote; nyumba yako haitakaribiwa na baa lolote. Maana Mungu atawaamuru malaika zake, wakulinde popote uendapo. Watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe. Utakanyaga simba na nyoka, utawaponda wana simba na majoka. Mungu asema: “Nitamwokoa yule anipendaye; nitamlinda anayenitambua! Akiniita, mimi nitamwitikia; akiwa taabuni nitakuwa naye; nitamwokoa na kumpa heshima. Nitamridhisha kwa maisha marefu, nitamjalia wokovu wangu.”
Zaburi 91:9-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa kuwa Wewe BWANA ndiwe kimbilio langu; Umemfanya Aliye Juu kuwa makao yako. Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako. Kwa kuwa atakuagizia malaika wake Wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Utawakanyaga simba na nyoka, Mwanasimba na joka utawakanyaga kwa miguu. Kwa kuwa amekaza kunipenda Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, Kwa kuwa amenijua Jina langu. Ataniita nami nitamwitikia; Nitakuwa pamoja naye taabuni, Nitamwokoa na kumtukuza; Kwa siku nyingi nitamshibisha, Nami nitamwonesha wokovu wangu.
Zaburi 91:9-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa kuwa Wewe BWANA ndiwe kimbilio langu; Umemfanya Aliye juu kuwa makao yako. Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako. Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Utawakanyaga simba na nyoka, Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu. Kwa kuwa amekaza kunipenda Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, Kwa kuwa amenijua Jina langu. Ataniita nami nitamwitikia; Nitakuwa pamoja naye taabuni, Nitamwokoa na kumtukuza; Kwa siku nyingi nitamshibisha, Nami nitamwonyesha wokovu wangu.
Zaburi 91:9-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kama ukimfanya Aliye Juu Sana kuwa makao yako: naam, BWANA ambaye ni kimbilio langu, basi hakuna madhara yatakayokupata wewe, hakuna maafa yataikaribia hema yako. Kwa kuwa atawaagiza malaika zake kwa ajili yako, wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuinua, ili usijikwae mguu wako kwenye jiwe. Utawakanyaga simba na nyoka wakali, simba mkubwa na nyoka utawaponda kwa miguu. BWANA asema, “Kwa kuwa ananipenda, nitamwokoa; nitamlinda, kwa kuwa analikiri Jina langu. Ataniita, nami nitamjibu; nitakuwa pamoja naye katika taabu, nitamwokoa na kumheshimu. Kwa siku nyingi nitamshibisha na kumwonyesha wokovu wangu.”