1 Wakorintho 13:1-7
1 Wakorintho 13:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Hata kama nikinena lugha za watu na hata za malaika, lakini kama sina upendo mimi nimekuwa tu kama sauti ya debe tupu au kengele. Tena, naweza kuwa na kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, nikafahamu siri zote na kujua kila kitu; naweza kuwa na imani yote hata nikaweza kuihamisha milima, lakini kama sina upendo mimi si kitu. Nikitoa mali yangu yote na kuwapa maskini, na tena nikiutoa mwili wangu uchomwe, kama sina upendo hiyo hainifai chochote. Mwenye upendo huvumilia, hufadhili; mwenye upendo hana wivu, hajidai, wala hajivuni. Mwenye upendo hakosi adabu, hatafuti faida yake binafsi, wala hana wepesi wa hasira; haweki kumbukumbu ya mabaya, hafurahii uovu, bali hufurahia ukweli. Mwenye upendo huvumilia yote, huamini yote, na hustahimili yote.
1 Wakorintho 13:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, mimi si kitu. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidi kitu. Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.
1 Wakorintho 13:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hata kama nitasema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa kengele inayolialia au toazi livumalo. Ningekuwa na karama ya unabii na kujua siri zote na maarifa yote, hata kama nina imani kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, mimi si kitu. Kama nikitoa mali yote niliyo nayo na kama nikijitolea mwili wangu uchomwe moto, kama sina upendo, hainifaidi kitu. Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi. Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli. Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.
1 Wakorintho 13:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu. Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.