Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 13:1-10

1 Wafalme 13:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

Siku moja Yeroboamu alikuwa amesimama kando ya madhabahu ili afukize ubani. Basi, mtu wa Mungu kutoka Yuda akawasili hapo Betheli na ujumbe wa Mwenyezi-Mungu. Mtu huyo akailaani ile madhabahu akisema, “Ee madhabahu! Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Atazaliwa mtoto katika ukoo wa Daudi, jina lake Yosia. Huyo atawatwaa makuhani wanaohudumu mahali pa ibada na kufukiza ubani juu yako, na kutambika juu yako; naam, mifupa ya watu itateketezwa juu yako!’” Mtu huyo akatoa ishara siku ileile, akasema: “Hii ndiyo ishara aliyotamka Mwenyezi-Mungu: ‘Madhabahu itabomoka, na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.’” Mfalme Yeroboamu aliposikia maneno hayo ya mtu wa Mungu dhidi ya madhabahu huko Betheli, alinyosha mkono akasema, “Mkamateni huyo!” Na mara huo mkono wake aliounyosha, ukakauka, asiweze tena kuukunja. Madhabahu nayo ikabomoka, na majivu yake yakamwagika chini, kama ishara ile aliyoitoa huyo mtu wa Mungu na ujumbe wa Mwenyezi-Mungu. Basi, mfalme Yeroboamu akamwambia nabii, “Tafadhali, umsihi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, uniombee mkono wangu upate kupona.” Naye nabii akamwomba Mwenyezi-Mungu, na mkono wa mfalme ukapona, ukarudia hali yake ya hapo awali. Ndipo mfalme akamwambia mtu wa Mungu, “Karibu nyumbani kwangu kula chakula, nami nikupe zawadi.” Lakini mtu wa Mungu akamwambia, “Hata kama ukinipa nusu ya milki yako, sitakwenda pamoja nawe. Sitakula wala kunywa maji mahali hapa, kwani Mwenyezi-Mungu aliniamuru nisile chakula au kunywa maji, wala nisirudi kwa njia ileile niliyoifuata kuja hapa.” Basi, mtu huyo akaenda zake, wala hakurudi kwa njia ile aliyoijia Betheli.

1 Wafalme 13:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Na tazama, akatoka mtu wa Mungu katika Yuda kwa neno la BWANA, akafika Betheli. Naye Yeroboamu alikuwa akisimama penye madhabahu, afukize uvumba. Basi mtu huyo akapiga kelele juu ya madhabahu, kwa neno la BWANA akasema, Ee madhabahu, madhabahu, BWANA asema hivi, Angalia, mtoto atazaliwa katika nyumba ya Daudi, jina lake Yosia; na juu yako atawatambika makuhani wa mahali pa juu, wanaofukiza uvumba juu yako, na mifupa ya watu itateketezwa juu yako. Akatoa ishara siku ile ile, akasema, Hii ndiyo ishara aliyoinena BWANA, Tazama, madhabahu itapasuka, na majivu yaliyo juu yake yatamwagika. Ikawa, mfalme Yeroboamu alipoyasikia maneno ya yule mtu wa Mungu, alipopiga kelele juu ya madhabahu huko Betheli, alinyosha mkono wake pale madhabahuni, akasema, Mkamateni. Basi ule mkono wake aliounyosha ukakatika, wala hakuweza kuurudisha kwake tena. Madhabahu ikapasuka, majivu ya madhabahuni yakamwagika, sawasawa na ishara aliyoitoa mtu wa Mungu kwa neno la BWANA. Mfalme akajibu, akamwambia yule mtu wa Mungu, Umsihi sasa BWANA, Mungu wako, ukaniombee, ili nirudishiwe mkono wangu tena. Yule mtu wa Mungu akamwomba BWANA mkono wa mfalme ukarudishwa tena, ukawa kama ulivyokuwa kwanza. Mfalme akamwambia mtu wa Mungu, Karibu nyumbani kwangu ujiburudishe, nami nitakupa thawabu. Mtu wa Mungu akamwambia mfalme, Ujaponipa nusu ya nyumba yako, sitaingia pamoja nawe, wala sitakula chakula, wala sitakunywa maji mahali hapa; maana ndivyo nilivyoagizwa kwa neno la BWANA, kusema, Usile chakula chochote wala usinywe maji, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia. Basi akaenda zake kwa njia nyingine, wala hakurudi kwa njia ile aliyoijia Betheli.

1 Wafalme 13:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Na tazama, akatoka mtu wa Mungu katika Yuda kwa neno la BWANA, akafika Betheli. Naye Yeroboamu alikuwa akisimama penye madhabahu, afukize uvumba. Basi mtu huyo akapiga kelele juu ya madhabahu, kwa neno la BWANA akasema, Ee madhabahu, madhabahu, BWANA asema hivi, Angalia, mtoto atazaliwa katika nyumba ya Daudi, jina lake Yosia; na juu yako atawachinja makuhani wa mahali pa juu, wanaofukiza uvumba juu yako, na mifupa ya watu itateketezwa juu yako. Akatoa ishara siku ile ile, akasema, Hii ndiyo ishara aliyoinena BWANA, Tazama, madhabahu itapasuka, na majivu yaliyo juu yake yatamwagika. Ikawa, mfalme Yeroboamu alipoyasikia maneno ya yule mtu wa Mungu, alipopiga kelele juu ya madhabahu huko Betheli, alinyosha mkono wake pale madhabahuni, akasema, Mkamateni. Basi ule mkono wake aliounyosha ukakatika, wala hakuweza kuurudisha kwake tena. Madhabahu ikapasuka, majivu ya madhabahuni yakamwagika, sawasawa na ishara aliyoitoa mtu wa Mungu kwa neno la BWANA. Mfalme akajibu, akamwambia yule mtu wa Mungu, Umsihi sasa BWANA, Mungu wako, ukaniombee, ili nirudishiwe mkono wangu tena. Yule mtu wa Mungu akamwomba BWANA mkono wa mfalme ukarudishwa tena, ukawa kama ulivyokuwa kwanza. Mfalme akamwambia mtu wa Mungu, Karibu nyumbani kwangu ujiburudishe, nami nitakupa thawabu. Mtu wa Mungu akamwambia mfalme, Ujaponipa nusu ya nyumba yako, sitaingia pamoja nawe, wala sitakula chakula, wala sitakunywa maji mahali hapa; maana ndivyo nilivyoagizwa kwa neno la BWANA, kusema, Usile chakula cho chote wala usinywe maji, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia. Basi akaenda zake kwa njia nyingine, wala hakurudi kwa njia ile aliyoijia Betheli.

1 Wafalme 13:1-10 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Kwa neno la Mwenyezi Mungu, mtu wa Mungu alifika Betheli kutoka Yuda wakati Yeroboamu alipokuwa amesimama kando ya madhabahu ili kutoa sadaka. Akapiga kelele dhidi ya madhabahu kwa neno la Mwenyezi Mungu: “Ee madhabahu, ee madhabahu! Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Mwana aitwaye Yosia atazaliwa katika nyumba ya Daudi. Juu yako atawatoa dhabihu makuhani wa mahali pa juu pa kuabudia ambao hutoa sadaka hapa, nayo mifupa ya wanadamu itateketezwa juu yako.’ ” Siku hiyo hiyo, mtu wa Mungu akatoa ishara: “Hii ndiyo ishara Mwenyezi Mungu aliyotangaza: Madhabahu haya yatapasuka na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.” Mfalme Yeroboamu aliposikia kile mtu wa Mungu alichosema, alipopiga kelele dhidi ya madhabahu huko Betheli, akanyoosha mkono wake kutoka madhabahuni na kusema, “Mkamateni!” Lakini mkono aliounyoosha kumwelekea yule mtu ukakauka kiasi kwamba hakuweza kuurudisha. Pia, madhabahu yakapasuka na majivu yakamwagika, sawasawa na ishara iliyotolewa na mtu wa Mungu kwa neno la Mwenyezi Mungu. Kisha mfalme akamwambia mtu wa Mungu, “Niombee kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ili mkono wangu upate kupona.” Kwa hiyo mtu wa Mungu akamwombea kwa Mwenyezi Mungu, nao mkono wa mfalme ukapona na kurudi ulivyokuwa hapo awali. Mfalme akamwambia yule mtu wa Mungu, “Twende nyumbani mwangu upate chakula, nami nitakupa zawadi.” Lakini yule mtu wa Mungu akamjibu mfalme, “Hata kama ungenipa nusu ya mali yako, nisingeenda pamoja nawe, wala nisingekula mkate au kunywa maji hapa. Kwa kuwa niliagizwa kwa neno la Mwenyezi Mungu: ‘Kamwe usile mkate wala usinywe maji au kurudi kwa njia uliyojia.’ ” Hivyo, akafuata njia nyingine na hakurudi kupitia njia aliyokuwa ameijia Betheli.