1 Wafalme 13
13
Mtu wa Mwenyezi Mungu kutoka Yuda
1Kwa neno la Mwenyezi Mungu, mtu wa Mungu alifika Betheli kutoka Yuda wakati Yeroboamu alipokuwa amesimama kando ya madhabahu ili kutoa sadaka. 2Akapiga kelele dhidi ya madhabahu kwa neno la Mwenyezi Mungu: “Ee madhabahu, ee madhabahu! Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Mwana aitwaye Yosia atazaliwa katika nyumba ya Daudi. Juu yako atawatoa dhabihu makuhani wa mahali pa juu pa kuabudia ambao hutoa sadaka hapa, nayo mifupa ya wanadamu itateketezwa juu yako.’ ” 3Siku hiyo hiyo, mtu wa Mungu akatoa ishara: “Hii ndiyo ishara Mwenyezi Mungu aliyotangaza: Madhabahu haya yatapasuka na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.”
4Mfalme Yeroboamu aliposikia kile mtu wa Mungu alichosema, alipopiga kelele dhidi ya madhabahu huko Betheli, akanyoosha mkono wake kutoka madhabahuni na kusema, “Mkamateni!” Lakini mkono aliounyoosha kumwelekea yule mtu ukakauka kiasi kwamba hakuweza kuurudisha. 5Pia, madhabahu yakapasuka na majivu yakamwagika, sawasawa na ishara iliyotolewa na mtu wa Mungu kwa neno la Mwenyezi Mungu.
6Kisha mfalme akamwambia mtu wa Mungu, “Niombee kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ili mkono wangu upate kupona.” Kwa hiyo mtu wa Mungu akamwombea kwa Mwenyezi Mungu, nao mkono wa mfalme ukapona na kurudi ulivyokuwa hapo awali.
7Mfalme akamwambia yule mtu wa Mungu, “Twende nyumbani mwangu upate chakula, nami nitakupa zawadi.”
8Lakini yule mtu wa Mungu akamjibu mfalme, “Hata kama ungenipa nusu ya mali yako, nisingeenda pamoja nawe, wala nisingekula mkate au kunywa maji hapa. 9Kwa kuwa niliagizwa kwa neno la Mwenyezi Mungu: ‘Kamwe usile mkate wala usinywe maji au kurudi kwa njia uliyojia.’ ” 10Hivyo, akafuata njia nyingine na hakurudi kupitia njia aliyokuwa ameijia Betheli.
11Basi kulikuwa na nabii fulani mzee aliyekuwa anaishi Betheli, ambaye wanawe walikuja kumwambia yote ambayo mtu wa Mungu alikuwa ameyafanya pale siku ile. Pia wakamwambia baba yao yale aliyomwambia mfalme. 12Baba yao akawauliza, “Ameelekea njia gani?” Nao wanawe wakamwonesha ile njia yule mtu wa Mungu kutoka Yuda aliyopita. 13Hivyo akawaambia wanawe, “Nitandikieni punda.” Walipokwisha kumtandikia punda, akampanda 14na kumfuatilia yule mtu wa Mungu. Akamkuta ameketi chini ya mwaloni na kumuuliza, “Je, wewe ndiwe mtu wa Mungu kutoka Yuda?”
Akamjibu, “Mimi ndiye.”
15Basi nabii akamwambia, “Karibu nyumbani pamoja na mimi, ule.”
16Yule mtu wa Mungu akasema, “Siwezi kurudi na kwenda nawe, wala siwezi kula mkate au kunywa maji pamoja nawe mahali hapa. 17Nimeambiwa kwa neno la Mwenyezi Mungu: ‘Kamwe usile mkate au kunywa maji huko au kurudia njia uliyojia.’ ”
18Yule nabii mzee akajibu, “Mimi pia ni nabii, kama wewe. Naye malaika alisema nami kwa neno la Mwenyezi Mungu: ‘Mrudishe aje katika nyumba yako ili apate kula mkate na kunywa maji.’ ” (Lakini alikuwa akimwambia uongo.) 19Hivyo mtu wa Mungu akarudi pamoja naye na akala na kunywa katika nyumba yake.
20Walipokuwa wameketi mezani, neno la Mwenyezi Mungu likamjia yule nabii mzee aliyemrudisha huyo mtu wa Mungu. 21Akampazia sauti yule mtu wa Mungu aliyekuwa ametoka Yuda, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Umeasi neno la Mwenyezi Mungu na hukushika amri uliyopewa na Mwenyezi Mungu, Mungu wako. 22Ulirudi, ukala mkate na kunywa maji mahali alipokuambia usile wala usinywe. Kwa hiyo maiti yako haitazikwa katika kaburi la baba zako.’ ”
23Huyo mtu wa Mungu alipomaliza kula na kunywa, nabii aliyekuwa amemrudisha akamtandikia punda wake. 24Alipokuwa akienda akakutana na simba njiani, akamuua na maiti yake ikabwagwa barabarani, huku punda wake na simba wakiwa wamesimama kando yake. 25Watu waliopita pale, waliona maiti iliyokuwa imebwagwa, simba akiwa amesimama kando yake. Nao wakaenda kutoa habari katika mji ambao nabii mzee alikuwa anaishi.
26Yule nabii aliyekuwa amemrudisha kutoka safari yake aliposikia habari hii akasema, “Ni yule mtu wa Mungu aliyeliasi neno la Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu amemtoa kwa simba, ambaye amemrarua na kumuua, sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu lilivyokuwa limemwonya.”
27Nabii akawaambia wanawe, “Nitandikieni punda,” nao wakafanya hivyo. 28Akaondoka na akakuta maiti imetupwa barabarani, punda na simba wakiwa wamesimama kando yake. Simba hakuwa amekula ile maiti wala kumrarua punda. 29Basi yule nabii mzee akachukua maiti ya mtu wa Mungu, akailaza juu ya punda na akairudisha katika mji wake, ili amwombolezee na kumzika. 30Kisha akailaza ile maiti katika kaburi lake huyo nabii mzee, nao wakaomboleza juu yake na kusema, “Ee ndugu yangu!”
31Baada ya kumzika, akawaambia wanawe, “Nitakapokufa, mnizike kwenye kaburi alimozikwa huyu mtu wa Mungu; lazeni mifupa yangu kando ya mifupa yake. 32Kwa maana ujumbe alioutangaza kwa neno la Mwenyezi Mungu dhidi ya madhabahu huko Betheli, na dhidi ya nyumba zote za ibada katika mahali pa juu pa kuabudia ndani ya miji ya Samaria, hakika utatimia.”
33Hata baada ya haya, Yeroboamu hakubadili njia zake mbaya, lakini mara nyingine tena akaweka makuhani kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia kutoka watu wa aina zote. Yeyote aliyetaka kuwa kuhani alimweka wakfu kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia. 34Hii ilikuwa ndiyo dhambi ya nyumba ya Yeroboamu ambayo iliisababishia kuanguka na kuangamia kwake hadi kutoweka kwenye uso wa dunia.
Iliyochaguliwa sasa
1 Wafalme 13: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.